Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua kanzi data itakayowezesha upatikanaji wa taarifa za fedha za wakopaji ili kuwatambua wafanyabiashara wanaokopa na kushindwa kurejesha fedha kwa wakati.
Benki hiyo itafanya kazi hiyo kwa kushirikiana kampuni ya Dun and Bradstreet Credit Bureau Tanzania Ltd.
Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa fedha wa BOT, Jerry Sabi amesema mfumo huo utaziwezesha taasisi za fedha kutoa mikopo kwa wingi.
Amesema BoT imeshatoa leseni kwa kampuni hiyo ili ianze kuandaa taarifa za wakopaji kutoka kwenye kanzidata ya Benki Kuu.
Ofisa wa kampuni hiyo, Miguel Llenas amesema mfumo huo utasaidia benki na taasisi zinazotoa mikopo kuwatambua wakopaji wasumbufu na kupunguza mikopo chechefu.
Amesema mfumo huo pia utaongeza uwajibikaji katika kukopesha na kukopa, pia kusaidia wakopeshaji na wadai kusimamia vitabu vyao vya mkopo, “na kuhakikisha viwango vya riba hulingana na maelezo husika ya mkopaji na kukuza bidhaa za mkopo katika soko la wakopeshaji.”
Pia Soma
- Msanii Harmonize asimulia alivyouza nyumba tatu kuwalipa Wasafi Sh500 milioni
- Bashungwa ataka washiriki kampuni 100 bora tangu mwaka 2011 kukutanishwa
- Waziri Biteko awapa somo wanajiolojia
Ameongeza, “inampa mkopeshaji taarifa sahihi za mchakato wa utoaji wa mikopo, ujumbe na mwongozo wa tathmini ya mkopaji, pia kuwezesha kasi ya utoaji mkopo na usimamizi wa wateja husika.”
"Pia mtoaji wa huduma anaweza kuongeza kasi ya upatikanaji wa wateja, kuelekeza na kusimamia mipaka ya mkopo yao na kuboresha utoaji wa huduma hizo.”
Akifafanua zaidi kuhusu huduma hizo meneja wa kampuni hiyo, Adebowale Atobatele amesema lengo lao ni kutoa suluhisho la usimamizi kuelekea mikopo isiyolipika katika sekta mbalimbali na kutoa taarifa sahihi kwa watoa mikopo kufanya maamuzi sahihi ya kutoa au kutokutoa.