Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki I&M kuwapa wateja wake mara mbili ya akiba yao

Tue, 2 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha wiki ya wateja, Benki I&M imetenga Sh75 milioni zitakazotolewa kwa wateja watakaoshinda promosheni ya benki hiyo itakayoendeshwa kwa miezi mitatu mfululizo.

Katika promosheni hiyo, benki hiyo imesema itampa kila atakayeshinda mara mbili ya akiba yake iliyopo kwenye akaunti muda husika.

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wa benki hiyo, Ndabu Swere alisema lengo la promosheni hiyo ijulikanayo kama jidabo ni kurudisha shukrani kwa wateja kutokana na uaminifu wao kwa taasisi hiyo ya fedha.

“Hii ni kwa wateja wote; waliopo na watakaofungua akaunti ndani ya kipindi cha promosheni. Ukiwa na akaunti ya mshahara, akiba, biashara au ya mtoto unashiriki moja kwa moja katika droo zitakazochezeshwa kila mwezi,” amesema Ndabu leo, Oktoba 2, 2018.

Kila mwezi, amesema wateja watano watapata bahati ya kushinda mara mbili ya akiba yao huku akibainisha kuwa kukidhi vigezo ni lazima mteja awe na walau Sh200,000 ingawa wateja wapya wanaweza kufungua akaunti kwa kiasi chochote wakawa wameingia moja kwa moja katika droo hiyo.

Tangu kuanzishwa kwa benki hiyo nchini mwaka 2010 imekuwa miongoni mwa benki zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma na kusikiliza wateja.

Kuhusu zawadi zitakazotolewa katika promosheni hiyo, meneja masoko na mawasiliano wa benki hiyo, Emmanuel Kiondo amesema kiasi cha juu ambacho mteja anaweza kushinda ni Sh10 milioni akimaanisha mteja anapaswa kuwa na Sh5 milioni na atakayekuwa na zaidi ya kiasi hicho atapewa Sh5 milioni ileile.

“Lengo ni kuwapa fursa wateja wadogo nafasi ya kushiriki promosheni na kuwa miongoni mwa washindi hao. Wengi husema promosheni hizi zinalenga watu wenye hela, tunataka kuwaonyesha tofauti yetu katika hilo,” amesema Kiondo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz