Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benki Exim yapata faida bilioni 6.58/-

97ecc508173d3b0b9407f56df00815d7.png Benki Exim yapata faida bilioni 6.58/-

Thu, 30 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya Exim imepata ongezeko la faida kabla ya kodi kwa asilimia 35 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka kilichoisha Juni 30, mwaka huu.

Mafanikio hayo yanatajwa kuwa yametokana na ufanisi kiutendaji licha ya changamoto za kiuchumi kutokana na ugonjwa wa covid-19.

Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Shani Kinswaga, ilionesha kuwa, benki hiyo imefanikiwa kupata faida ya Sh bilioni 6.58 katika robo ya pili ya mwaka huu, ikilinganishwa na faida ya Sh bilioni 4.90 kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.

"Tunafurahi kuripoti matokeo mazuri kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2020 licha ya athari kubwa ya janga la covid-19 kwenye uchumi.” “Tumerejesha asilimia nane kwenye mfuko wa wanahisa. Tunayachukulia mafanikio haya kama chachu ya kuendelea kufanya vizuri ili kutimiza malengo yetu na ya wateja wetu,” alisema.

Kinswaga alisema benki hiyo imeshirikiana kikamilifu na sekta zilizoathirika zaidi kiuchumi kutokana na janga la Covid-19 katika kuhakikisha zinajikwamua kwenye changamoto ya kifedha baada ya kuathirika na janga hilo.

Alisema Juni 2020, Benki ya Exim ilitoa msamaha wa zaidi ya Sh bilioni 160 kwa njia ya likizo ya malipo na upanuzi wa vipindi vya ulipaji wa mikopo ili kusaidia wateja wa benki hiyo ambao biashara zao zilizoathirika zaidi na athari za kiuchumi kutokana na covid-19.

"Jumla kuu ya mali zetu zote imebaki kuwa Sh trilioni 1.8, ikichangiwa hasa na ongezeko la asilimia tatu ya amana za wateja wetu katika kipindi hiki cha robo ya pili ya mwaka, hivyo kufanya jumla ya amana zote za wateja wetu kuwa Sh trilioni 1.33. Shughuli zetu nchini Tanzania, Comoro na Uganda zote zimerekodi ukuaji wa amana za wateja wakati wa robo hii."

"Benki imerekebisha mkakati wake wa muda wa kati kutokana na changamoto ya covid-19 kwa lengo la kuendeleza kasi ya ukuaji. Mkakati huo unategemea rasilimali watu, mchakato na teknolojia katika kukuza ukuaji endelevu. Matokeo ya robo hii ni ushahidi wa maendeleo yaliyofanywa," alisema.

Aidha, Kinswaga alisema katika kipindi hicho cha robo mwaka, Benki ya Exim ilizindua kampeni yake ya ‘Maliza Kirahisi Kidigitali', inayolenga kuhamasisha wateja wake kutumia zaidi huduma za kidigitali ili kurahisha upatikanaji wa huduma na kuokoa muda ambao wangeutumia kwenda kwenye matawi ya benki hiyo.

Alisema kampeni hiyo imekuja kipindi ambacho jamii inapitia mabadiliko kuelekea huduma za kidigitali hususan katika huduma za kifedha na manunuzi, hali iliyochochewa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa covid-19.

Pia alisema katika kutekeleza mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) unaofahamika kwa jina "Exim Cares", benki hiyo ilikabidhi msaada ya vyakula na vifaa kinga dhidi ya maambukuzi ya virusi vya corona kwa vituo vinne vya kulelea yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Mtwara na Tanga.

Chanzo: habarileo.co.tz