Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei za vyakula zapaa msimu wa kilimo ukianza

90424 Vyakula+pic Bei za vyakula zapaa msimu wa kilimo ukianza

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bei za mazao makuu ya chakula zimeanza kupanda wakati msimu wa mvua ukianza katika mikoa mbalimbali nchini.

Maharage yanayotumika katika mlo wa familia nyingi, sasa yanaongoza kwa kwa kupanda bei kwa angalau asilimia 25 ndani ya miezi mitatu iliyopita.

Uchunguzi uliofanywa katika masoko ya jumla na na rejareja jijini umeonyesha kwamba maharage sasa yanauzwa hadi Sh3,200 kwa kilo kutoka Sh2400 bei ya Oktoba.

Pia nafaka za mchele na mahindi zinaonekana kuongezeka bei japo kwa taratibu katika miezi ya hivi karibuni, kwa mujibu wa wafanyabiashara.

Wafanyabiashara wanasema kupanda huko ni hali ya kawaida kutokana na misimu na mahitaji yaliyotokana na sikukuu za mwisho wa mwaka. Wamesema pia kutopatikana kwa mazao hayo sokoni hakuhusiani na upatikanaji wa chakula nchini.

“Kwa maharage, ni kawaida kupanda na kushuka. Katika miezi mitatu iliyopita tumeshuhudia kupungua kwa upatikanaji wake na ndiyo maana bei zimekuwa zikipanda,” alisema Adan Msury ambaye ni muuza nafaka katika soko la Double Cabin la Temeke.

“Tunaamini bei zitashuka ifikapo Januari kwa sababu kutakuwa na mavuno mengine ya maharage kutoka mikoa kama Kagera, kwa hiyo yataongezeka,” aliongeza.

“Kitu cha kuchekesha kuhusu maharage ni kwamba bei yake inaweza kupanda kwa miezi mitatu, halafu ikashuka ghafla. Hapo ndipo tunakula mitaji yetu,” alisema.

Wafanyabiashara pia wamesema mvua zinazoendelea kunyesha zimechangia kupanda bei kwa bidhaa hizo kutokana na usafirishaji wake kutoka mikoani kuwa na changamoto nyingi.

“Tanzania ina chakula cha kutosha, lakini tatizo lipo katika usafirishaji kutoka mikoani. Mvua nyingi zinazonyesha zinakwamisha usafirishaji kutoka maeneo ya vijijini,” alisema Mohamed Mwekya ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Tandale.

“Tunatakiwa kuelewa kuwa akiba ya mazao hayo ilikuwa chini ya madalali, yaani wafanyabiashara walionunua na kuhifadhi wakisubiri bei zifikie mahali pa kuwapa faida,” alisema Mwekya.

Alisema hali hiyo ni ya muda kwani inaweza kudumu kwa mwezi mmoja au miwili ijayo.

Tabran Shabani, anayeuza mahindi katika soko la Manzese, anasema zao hilo lilipanda bei hadi Sh1,000 kwa kilo kabla hayajakobolewa au kusagwa.

“Hiki ni kipindi kigumu sana katika msimu wa kupanda kwa bei kutokana na kutopatikana kwa mazao. Mashine nyingi tu zimefungwa hapa Manzese kwa sababu inabidi uwe makini kuendesha mashine hizo,” alisema.

“Kwa uzoefu wangu, bei ya mahindi itaendelea kupanda hadi mwisho wa Februari wakati ambao maeneo kama Kahama wataanza kuleta mahindi,” aliongeza.

Anauza mahindi kwa Sh35,000 kwa gunia la kilo 25 wakati wauzaji wa rejareja wanauza Sh1,600 kwa kilo.

Mchele pia unauzwa kati ya Sh1700 na Sh2300 maeneo ya Mbagala.

“Kwa sasa nategemea kupata mchele kutoka Mbeya ambako pia bei zinapanda,” alisema Ali Omary anayeuza nafaka Mbagala.

“Nadhani bei itaendelea kupanda hadi Machi ambapo kutakuwa na mavuno mengine yatakayoingia kutoka Kanda ya Ziwa hasa Shinyanga.”

Taarifa kutoka soko la Kariakoo zinasema bei za vyakula zimepanda kwa kasi ndani ya mwaka mmoja kwa mazao yote.

Chanzo: mwananchi.co.tz