Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei za nauli Ubungo zaanza kupandishwa kiholela

32850 Pic+ubungo Tanzania Web Photo

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka hali ya usafiri katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam imeanza kubadilika baada ya abiria kupandishiwa nauli kiholela.

Hayo yamebainika leo Jumamosi Desemba 22,2018 baada ya waziri wa  ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, Isaack Kamwelwe kufanya ziara kituoni hapo kuona hali ya usafiri.

Waziri Kamwele amefika kitoni hapo saa 11:15 alfajiri na kuzunguka kwenye baadhi ya mabasi na kubaini baadhi ya abiria kulipishwa nauli tofauti.

"Katika ukaguzi niliofanya nimebaini abiria kulipa nauli tofautitofauti, hii ni kutokana nakuwepo kwa madalali nje ya kituo," amesema Waziri Kamwelwe

Amesema kuna haja ya kupeleka mapendekezo bungeni ili kuwepo kwa tiketi za mfumo wa kielektroniki zitakazosaidia kuepuka  ulanguzi.

Baadhi ya abiria wamesema kinachosababisha nauli ipande ni madalali wanaokatisha tiketi nje ya kituo. Mfano nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha imepanda kutoka Sh28,000 hadi Sh35,000.

Joseph Malisa amesema unapokwenda kwenye ofisi au gari husika unaambiwa gari limejaa lakini nje ya kituo unakuta madalali wanauza tiketi.

"Unapofika kwenye gari au ofisi zao unaambiwa nafasi zimejaa lakini nje ya kituo madalali wanauza tiketi kwa bei ya juu," amesema Malisa

Emili Msuya amesema kupanda kwa nauli kiholela kumechangiwa na watu wasio rasmi ikiwemo wapiga debe wanaolundikana ndani ya kituo hivyo serikali iangalie utaratibu wa kuwaondoa.

Meneja wa kituo cha Ubungo Imani Kasagala amesema mabasi yote yanapaswa kuingia ndani ya Ubungo badala ya wamiliki kupaki nje na kutafuta madalali ambao ndio chanzo cha kupanda kwa nauli.

Soma zaidi: Hali ya usafiri jijini Arusha ni shwari

 



Chanzo: mwananchi.co.tz