Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei za nafaka masokoni zapungua asilimia tano

69580cb7c5a824bcd6253a95798aa9da Bei za nafaka masokoni zapungua asilimia tano

Thu, 14 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WASTANI wa bei za nafaka katika masoko mbalimbali nchini zimepungua kwa asilimia tano, huku bei ya viazi mviringo na mazao ya viungo na matunda zikiongezeka hadi asilimia 12.

Kwa mujibu wa taarifa ya wiki ya mwenendo wa bei za mazao ya chakula iliyotolewa na Wizara ya Kilimo, Sehemu ya Masoko ya Mazao ya Kilimo, bei hizo zimebadilika kati ya Desemba mwaka jana na Januari 8, mwaka huu.

Katika mwenendo huo, wastani wa bei za mahindi na mtama kitaifa hazijabadilika, ambapo kuanzia Desemba 28, mwaka jana gunia la kilo 100 limeendelea kuuzwa kwa Sh 57,000 hadi kufikia Januari 8, mwaka huu.

Aidha, gunia la mtama la kilo 100 limeendelea kuuzwa kwa Sh 88,000 kwa kipindi hicho, wakati maharage na mchele bei zimepungua kwa asilimia tano na bei ya viazi mviringo ikiongezeka kwa asilimia sita.

Bei ya mchele hivi sasa gunia la kilo 100 linauzwa kwa wastani wa Sh 141,350 kutoka wastani wa Sh 149,000 katika mikoa mingi isipokuwa maeneo ya Mpanda (Katavi) na Musoma (Mara) ambako bei ya gunia moja ni wastani wa Sh 96,000.

Kwa zao la maharage, gunia la kilo 100 hivi sasa linauzwa kwa wastani wa Sh 197,000 kutoka Sh 207,000 Desemba mwaka jana, lakini mkoani Dar es Salaam bei ya zao hilo katika soko la Tandika imeendelea kubaki ile ile ya Sh 260,000 kwa gunia la ujazo huo tangu Desemba 21, mwaka jana.

“Bei za baadhi ya mazao ya nafaka zimeendelea kubaki kama zilivyokuwa lakini nafaka nyingine zimepungua bei hadi asilimia tano na nafaka hizo ni kama vile maharage na mchele,” ilisema sehemu ya taarifa hizo.

Viazi mviringo katika masoko mbalimbali nchini imeongezeka kwa wastani wa asilimia sita, ambapo katika soko Arusha Mjini gunia moja la kilo 100 linauzwa kwa Sh 77,500 hivi sasa kutoka Sh 69,000 Desemba 28, mwaka jana.

Kwenye mazao ya viungo na matunda, hali imebadilika ambapo katika wiki ya kwanza ya Januari mwaka huu bei imeongezeka kwenye mazao ya nyanya, vitunguu maji, tikiti maji, nanasi, pilipili hoho na matango.

Kreti moja la nyanya la kilo 40 linauzwa Sh 33,400 wakati Desemba mwanzoni mwaka jana lilikuwa likiuzwa kwa Sh 27,000, bei ya vitunguu maji imeongezeka kwa asilimia moja kutoka Sh 89,000 hadi Sh 90,600, huku bei ya pilipili hoho ikiongezeka kutoka Sh 44,000 kwa gunia la kilo 50 hadi Sh 46,000 kwa ujazo huo.

Chanzo: habarileo.co.tz