Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya tumbaku yaongeza hamasa kwa wakulima

Zimbabwe Yajivunia Mavuno Ya Tumbaku 2023 Bei ya tumbaku yaongeza hamasa kwa wakulima

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ongezeko la bei ya tumbaku kutoka Dola 1.85 za Marekani (Sh4,625) hadi dola 2.44 (Sh6,100) kwa kilo limetajwa kuchochea hamasa kwa wakulima wa zao hilo wilaya hapa.

Katika kuhakikisha wakulima wanaendelea kunufaika, Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Chunya (Chutcu), kimepanga kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni 18 kwa msimu wa 2022/23, mpaka kilo milioni 27.2 kwa msimu wa 2023/24.

Mikoa ya Mbeya na Songwe ni miongoni mwa inayolima tumbaku kwa Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini ambapo, Chutcu na Vyama vya Msingi (Amcos) 33 vyenye wakulima 7,200 vimekuwa vikishirikiana kuhakikisha uzalishaji unaongezeka.

Meneja wa Uzalishaji wa Chutcu, Juma Shishi amelieleza Mwananchi jana Alhamis, Novemba 23,2023, amesema mwamko wa wakulima msimu huu umekuwa maradufu tofauti na uliopita.

“Hamasa imekuwa kubwa kwa wakulima, ndio sababu msimu huu tumeweka malengo kwa uzalishaji kufikia kilo milioni 27.2 kutoka kilo milioni 18 za mwaka jana,” amesema Shishi.

Katika kuhakikisha wanafikia malengo hayo, Shishi amesema wamepanga kutoa elimu kwa wakulima kuzingatia taarifa za hali ya hewa, kuandaa mashamba kwa kufuata ushauri wa kitaalamu pamoja na kupanda miti ambayo itatumika kukausha zao hilo baada ya kuchoma.

Naye Meneja Mkuu wa Chutcu, Christian Msigwa amesema ili kufikia malengo hayo wamepokea asilimia 30 ya pembejeo za kilimo huku dawa zikiwa ni asilimia 80 na tayari zimesambazwa kwa wakulima hasa maeneo ya pembezoni.

“Bado mahitaji ya mbolea ni makubwa lakini tunaendelea kupokea ifikapo Desemba tutakuwa tumetimiza kwa asilimia 100 na kukidhi mahitaji ya matarajio ya kuzalisha kilo milioni 27.2. Pia tumeenda kuhamasisha wakulima kuendelea kuzalisha mahindi na alizeti kwa ajili ya chakula,” amesema.

Amesema kufuatia hali hiyo Chutcu wamejenga kiwanda cha kuchakata mazao ya mahindi na alizeti ili wakulima wazalishe kwa tija mazao mbadala ya kibiashara.

Msigwa amesema kwa kuzingatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) tayari wakulima wamepatiwa elimu ya tahadhari wapandapo tumbaku, wahakikishe kwenye mashamba kuna miche ya mahindi na alizeti.

“Unajua namna tumbaku inavyostawi inahitaji uwepo wa mazao mengine endapo kutakuwa na mvua nyingi hivyo ni wakati sasa wakulima kutumia mbinu hiyo ili kuepuka majanga,” ameongeza.

Ofisa Kilimo Wilaya ya Chunya, Cuthbert Mwinuka amesema katika msimu uliopita wakulima walizalisha tumbaku kidogo kutokana na changamoto ya mvua na uhaba wa mabani.

“Msimu uliopita zaidi kilo milioni sita zilipotea kutokana na mabani kubomoka kwa kushindwa kumudu wingi wa maji ya mvua,” amesema.

Amesema kwa Chunya pekee mahitaji ya mabani ya kukaushia tumbaku ni 88,000 huku yaliyopo ni 44,000 ambayo hayakidhi mahitaji ya uzalishaji wa kilo kuanzia milioni 27 hadi 30.

Kutokana na hilo, wameanza mazungumzo na taasisi za kifedha kuona namna bora ya kutoa mikopo ili kusaidia wakulima kuepuka hasara kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Lupa, Masingija Jilala amesema wametenga zaidi hekari zaidi 30,000 za miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku kwa msimu ujao huku utunzaji wa mazingira ukipewa kipaumbele.

“Tuna utaratibu wa ‘panda mti, kata mti’ na sasa tumepanda kwa wakati kwa kutumia mvua za mwanzo ili baadaye kusiwepo madhara na kuhamasisha wakulima kupanda miti kila msimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live