Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya sukari yapaa sokoni, Serikali yaagiza tani 40,000

102247 Pic+sukari Bei ya sukari yapaa sokoni, Serikali yaagiza tani 40,000

Mon, 13 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Bei ya sukari katika mikoa mbalimbali imeongezeka kwa kati ya Sh300 na Sh700, huku Waziri wa Kilimo akitaja sababu ya ongezeko hilo na kuwatoa hofu wananchi kwani tani 40,000 zimeshawasili kurekebisha hali hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa bidhaa hiyo imepanda bei kwa takribani mwezi mmoja sasa, lakini kuna tofauti ya ongezeko hilo katika maeneo.

Katika baadhi ya maeneo, bei imepanda kutoka Sh2,600 kwa kilo moja hadi Sh3,000 na maeneo mengine kutoka Sh2,800 hadi Sh3,000, huku katika mikoa kama Arusha, Mwanza na Dodoma bei imepanda kutoka kati ya Sh2,400 kwa kilo moja hadi Sh3,000 na vijijini imefika Sh3,500.

“Ni kweli bei ya sukari imeanza kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake, lakini Serikali tayari imeagiza tani 40,000 kutoka nje ya nchi ili kumaliza changamoto hiyo,” alisema Waziri wa Kilimo, Joseph Hasunga.

“Kwa kawaida viwanda vyote huwa vinasimamisha uzalishaji mwezi Mei ili kufanya ukarabati, lakini mwaka huu imekuwa tofauti vimesimamisha miezi miwili kabla ya muda uliopangwa kwa sababu mashamba ya miwa yamejaa maji kutokana na mvua zilizonyesha kwa wingi.”

Alisema sukari iliyoagizwa ni kwa ajili ya kufidia upungufu uliopo kwa kipindi ambacho uzalishaji utakuwa umesimama. Alisema kulikuwa kuna uchelewaji katika kuitoa bandarini, lakini punde itaingizwa katika mzunguko.

Pia Soma

Advertisement
Alisema Serikali inaendelea kutathmini mwenendo wa upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu na kama italazimika, itaagiza shehena nyingine.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wafanyabiashara walisema kupanda kwa bei kumeshabishwa na kupungua uzalishaji viwandani na hofu ya kukosekana madukani iwapo Serikali itatangaza kuzuia watu kutoka nyumbani kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

“Bei ilianza kupanda tangu wiki iliyopita kutoka Sh130,000 kwa kilo 50, hadi Sh165,000. Kulikuwa na akiba ndogo,” alisema Shirima, mkazi wa Sakina.

“Wanasema kuna viwanda vinafungwa ili kufanyiwa usafi kabla ya kuanza msimu mpya na wengine wanasema mahitaji ya sukari katika nchi jirani pia yamechangia wafanyabiashara wakubwa kusafirisha.”

Hofu ya marufuku ya kutoka nje pia ilitajwa na John Laizer, ambaye pia anauza bidhaa hiyo.

“Mimi hapa dukani nilikuwa na kilo 150 sasa nimebakiza kilo chini ya 15. Watu wananunua kwa wingi licha ya bei kupanda hadi Sh3,000 kwa kilo,” alisema.

Lakini mkoani Katavi kulikuwa na sababu nyingine ya ongezeko la bei ya sukari.

Wafanyabiashara wanaamini kuwa kufungwa kwa muda kwa usafiri wa barabara na reli kati ya Tabora - Mpanda ni moja ya sababu kuu za ongezeko hilo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Diana John alisema bei ya sukari imepanda takribani mwezi mmoja sasa na upatikanaji wa wateja ni mgumu.

“Mfuko wa sukari kilo 25 kwa bei ya jumla tunanunua Sh64,000 hadi 65,000 wakati awali tulikuwa tunanunua Sh60,000 hadi Sh61,000,” alisema.

“Bei imepanda sana, nadhani uzalishaji umeshuka kutokana na janga hili la corona.”

“Lakini kufungwa barabara ya Tabora- Mpanda pamoja na reli kumechangia kupanda bei. Niiombe Serikali iongeze usimamizi ili matengenezo yakamilike na kiwandani walegezewe masharti ya mikusanyiko ili waongeze uzalishaji.”

Mjini Sengerema imepanda kutoka Sh2,400 hadi Sh3,000.

Mmoja wa wafanyabiashara mjini humo, Juma Magesa alisema mfuko wa kilo 50 kwa sasa wananunua kwa Sh127, 000 kutoka Sh124,000, na ule wa kilo 25 wananunua kwa Sh66,000 tofauti wakati awali ilipokuwa Sh64,000.

Tofauti si kubwa sana wilayani Serengeti ambako sukari imepanda kutoka Sh2,500 hadi Sh2,800 kwa kilo.

Mkoani Mwanza, mmiliki wa duka la nafaka katika kata ya Butimba, Marco Mushi alisema kwa sasa wananunua mfuko wa kilo 50 kwa Sh126,000 badala ya bei ya Sh107,000 za awali.

Mushi alisema wanalazimika kuuza sukari kwa bei ya Sh3,000 badala ya bei ya awali kutokana na wauzaji wa jumla kupandisha bei.

Hali ni hiyo hiyo mjini Kahama mkoani Shinyanga, ambako John Gibson, mkazi wa Nyahanga, anasema wananunua mfuko wa kilo 25 kwa Sh74,000 badala ya Sh56,000 huku mfuko wa kilo 20 wakinunua kwa Sh61,000 kutoka Sh49,000.

“Bei ya kilo moja imepanda kutoka Sh2,500 hadi Sh2,800,” alisema muuzaji huyo wa sukari kwa rejareja.

Ingawa ongezeko si kubwa mkoani Tabora, lakini bei ya kilo moja imefikia kiwango kinachofanana na maeneo mengine. Kilo moja imepanda kwa Sh200 tu, lakini imefikia kati ya Sh2,900 na Sh3,000.

Siku tatu zilizopita kilo moja ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh2,700 hadi Sh2,800.

Wilayani Kasulu mkoani Kigoma pia bei imepanda kwa Sh200 tu lakini imefikia Sh3,000 kama mikoa mingine. Bei ya sukari imepanda hadi Sh59,500 kutoka Sh58,000 kwa mfuko kwa kilo 50 kwa bei ya jumla huku bei ya reja reja ikiwa ni Sh60,500 na kilo moja ikiuzwa Sh3,000 kutoka Sh2,800.

Hata hivyo maeneo mengi ya Kigoma mjini bei imeendelea kuwa kati ya Sh2,600 na Sh2,800 kulingana na eneo.

Mkoani Dodoma, Athuman Maulid anayefanya biashara Soko la Sabasaba alisema bei ya sukari kwa sasa imepanda, hivyo ili wapate faida na wao wameamua kupandisha bei hiyo.

Alisema awali walikuwa wananunua mfuko wa kilo 50 kwa Sh148,000 hadi Sh150,000 lakini kwa sasa wananunua mfuko huo kwa Sh155,000.

“Ukiona bidhaa imepanda bei huku kwetu, ujue huko tunakotoa pia wameongeza bei. Hatuwezi kuendelea kuuza bei ile ile ya zamani wakati katika maduka ya jumla imepanda,” alisema Maulid.

Mjini Songea kuna ongezeko la Sh500 kwa kilo moja ya sukari. Awali bei ilikuwa Sh2,500 lakini sasa kilo inauzwa Sh3,000, lakini ofisa biashara mkoani Ruvuma, Nehemia James amewaonya wafanyabiashara wanaopandisha bei.

James amesema sukari inatakiwa iuzwe kati ya Sh2,500 hadi 2,600 kwa kilo.

Imeandikwa na Ephrahim Bahemu, Mary Clemence, Joyce Joliga, Rachel Chibwete, Daniel Makaka, Anthony Mayunga, Stella Ibengwe, Jesse Mikofu, Sada Amir, Robert Kakwesi, Suzy Butondo, Alodia Dominick, Diana Rubanguka, Mussa Juma na Happiness Tesha

Chanzo: mwananchi.co.tz