Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya samaki ‘kaa la moto’ kwa wamiliki wa viwanda

Wed, 24 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Siku tano baada ya Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), kutangaza mgomo wa muda usiojulikana wa kutoendelea na uvuvi pamoja na kusitisha kupeleka samaki kwenye viwanda vya kuchakata samaki aina ya sangara, Serikali imetoa msimamo wake.

Msimamo huo umetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyeviagiza viwanda hivyo kuendelea kununua samaki kwa bei ya awali ambayo ni ya juu ya Sh8,000 badala ya Sh4,500 waliyokuwa wakitaka kununulia sasa.

Akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha wamiliki wa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki, wawakilishi wa vyama vya wavuvi, wavuvi, mawakala na wafanyabiashara wa samaki jijini Mwanza mwishoni mwa wiki, Mpina alisema iwapo wamiliki hao wasipozingatia amri hiyo, Serikali itaamuru vinginevyo. “Serikali haikubaliani na uamuzi wa kushusha bei, hivyo wenye viwanda bado mnayo nafasi kabla Serikali haijawapangia,” alisema Mpina.

Masoko ya Uganda na Kenya

Akizungumzia kuhusu mawazo ya wafanyabiashara kuuza samaki kwenye masoko ya Uganda na Kenya, waziri huyo alisema yanakwenda kinyume na sera ya Serikali inayohimiza viwanda.

Awali, wamiliki wa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki katika mwambao wa Ziwa Victoria walimweleza waziri kuwa wameshusha bei ya samaki kutokana na soko la nje kuporomoka na kujikuta wanapata hasara.

Wiki moja iliyopita, Tafu walitangaza mgomo wa muda usiojulikana wa kutoendelea na uvuvi na uuzaji wa samaki kwenye viwanda vya uchakataji.

Msemaji wa chama hicho, Sijaona James alisema wameamua kusitisha shughuli hiyo baada ya bei kushuka kutoka Sh8,000 kwa kilo mwaka jana na kufikia Sh4,500 kwa sasa. Alisema hali hiyo imesababisha kudorora kwa biashara na hailingani na gharama za uzalishaji.

“Kuanzia leo tunasitisha kupeleka Samaki kwenye viwanda vya kuchakata minofu ya samaki hadi pale utaratibu mwingine utakapotangazwa, kwa sababu bei wanayotupa haitulipi na kwa wavuvi walio na samaki watawauza kwenye masoko ya kawaida kwa bei zitakazokuwepo,” alisema James.

Kauli ya kiongozi huyo iliungwa mkono na wavuvi ambao ni mawakala wa kuuza samaki kwenye viwanda hivyo.

Walielekeza lawama kwa wamiliki wa viwanda vya uchakataji samaki vya Kanda ya Ziwa kushusha bei huku vya nchi jirani vikinunua kwa bei ya juu.

Chanzo: mwananchi.co.tz