Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya petroli, dizeli yapanda Tanzania

94507 Pic+mafuta Bei ya petroli, dizeli yapanda Tanzania

Wed, 5 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza ongezeko la bei kwa mafuta yanayoingilia Bandari ya Dar es Salaam.

Mabadiliko hayo yanatokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani na ongezeko la bei katika soko la dunia.

Taarifa ya Ewura kwa mwezi Februari, 2020  inaonyesha lita moja ya petroli imepanda kwa Sh20 huku dizeli ikiongezeka kwa Sh74 na mafuta ya taa Sh44.

Ikilinganishwa na bei zilizokuwapo Januari 2020, bei za jumla ya petroli imeongezeka kwa Sh20.01 kwa lita, dizeli imeongezeka Sh74.21 na mafuta ya taa Sh43.96 kwa lita moja.

Licha ya mikoa inayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam, kanda ya kaskazini inayopokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga nako bei imepanda.

Kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, bei ya rejareja ya petroli imeongezeka kwa Sh42 kwa lita wakati mafuta ya taa yakipanda kwa Sh2 lakini dizeli ikishuka kwa Sh18.

Pia Soma

Advertisement
Bei ya jumla ya petroli imeongezeka kwa Sh41.94 na mafuta ya taa kwa Sh2.37 kwa kila lita moja ikilinganishwa na bei za Januari huku dizeli ikishuka kwa Sh17.49.

Kanda ya kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma bei za rejareja ya petroli imepanda kwa Sh35 wakati dizeli ikishuka kwa Sh22. Ikilinganishwa na Januari, bei ya jumla ya petroli imepanda kwa Sh35.27 kwa lita katika kanda hiyo.

“Kwa kuwa hakuna mafuta ya taa yaliyopelekwa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauri kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Ewura.

Bei ya rejareja ya mafuta ya taa katika mikoa hiyo, Ewura imesema itatokana na gharama za kusafirishwa kutokea Dar es Salaam hadi mkoa husika.

Kutokana na mbadiliko hayo, Ewura inawataka wamiliki wa vituo vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa zao na kubandika kwenye mabango yanayoonekana bayana.

Chanzo: mwananchi.co.tz