Bei ya mchele imefikia viwango vyake vya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika takriban kipindi miaka 15 iliyopita huku kukiwa na wasiwasi juu ya ugavi wa kimataifa wa bidhaa hiyo baada ya muuzaji mkuu, India, kuweka vizingiti katika uuzaji nje zao hilo muhimu. Hali mbaya ya hewa katika eneo la Kusini-Mashariki mwa Asia imeathiri zaidi uzalishaji mpunga.
Kulingana na data ya Chama cha Wauzaji Nje Mchele nchini Thailand, bei ya mchele mweupe wa Thailand uliovunjika kwa asilimia tano, imepanda hadi dola 648 kwa tani, kiwango chake cha juu zaidi tangu Oktoba 2008.
Ongezeko hilo linakuja baada ya msafirishaji mkuu wa mchele duniani, India, kutangaza vizuizi kwa usafirishaji wa mchele mweupe usio wa basmati mwishoni mwa Julai. Serikali ya India ilielezea hatua hiyo kama jaribio la kutuliza bei ya mchele wa ndani, ambayo imepanda kwa zaidi ya 30% tangu Oktoba 2022. Hata hivyo, marufuku hiyo imezua wasiwasi wa mfumuko wa bei zaidi kwenye soko la chakula duniani kwani mchele ni muhimu kwa lishe ya mabilioni ya watu wa Asia na Afrika.
Tishio la hivi sasa kwa usambazaji wa mchele linatoka Thailand, msafirishaji wa pili kwa ukubwa duniani, ambapo mamlaka zimekuwa zikiwahimiza wakulima kubadili mimea inayohitaji maji kidogo huku nchi ikikabiliana na hali kavu zaidi na kuanza kwa mfumo wa hali ya hewa wa El Nino. Mfumo wa mzunguko wa hali ya hewa unaelekea kupunguza mvua Kusini-Mashariki mwa Asia na maeneo mengine, na utaandamana athari hasi kwa mazao.
El Nino ya awali katika mwaka wa mazao wa 2015/16 ilipunguza kwa asilimia 16 pato la ekari ya mpunga ya Thailand. Kwa mujibu wa taariza wa taasisi ya kitaalamu ya Gro Database, Jumla ya mvua mwaka huu katika mikoa inayolima mpunga nchini Thailand inafikia 23% chini ya viwango vya mwaka jana, ingawa bado inakaribia wastani wa miaka 10.