Menu ›
Biashara
Tue, 5 Feb 2019
Chanzo: mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), inatangaza bei mpya za mafuta ambazo zimepungua ikilinganishwa na mwezi uliopita. Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Februari 5, 2019 na kaimu mkurugenzi wa Ewura, Nzinyangwa Mchany inasema bei hizo mpya zitaanza kutumika kuanzia kesho Jumatano Februari 6, 2019. |
Inaeleza kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta yaliyoingizwa nchini Tanzania kupitia Bandari ya Dar es Salaam, zimepungua kwa viwango tofauti. Inaonyesha kuwa wateja wa rejareja watapata unafuu wa Sh175 kwa lita ya petroli wakati wale wa dizeli wakishushiwa kwa Sh144 na mafuta ya taa Sh156. Hata kwa bei za jumla, petroli imepungua kwa Sh174.03 kwa lita, dizeli kwa Sh143.65 na mafuta ya taa Sh155.32 na kueleza kuwa kupungua kwa bei hizo kunatokana na kuendelea kushuka kwa bei katika soko la dunia. Licha ya mabadiliko hayo ya bei, mikoa ya kaskazini itabaki kama mwezi uliopita kutokana na kuwapo kwa shehena iliyopokelewa Januari, 2019 kupitia Bandari ya Tanga huku kukiwa bado kuna akiba kubwa iliyoingizwa Desemba 2018 Inafafanua kuwa bei za mafuta kwa mikoa ya kusini zilikokotolewa kulingana na gharama za mafuta yaliyopokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam lakini wiki ya pili ya Januari Bandari ya Mtwara ilipokea shehena ya petroli hivyo kubadili ukokotozi. Kwamba kuanzia Januari 25, 2019 bei ya rejareja ya petroli na dizeli katika mikoa hiyo zilikokotolewa kwa gharama za Bandari ya Mtwara hivyo zitaendelea kubaki kama zilizvyo kuanzia tarehe hiyo. |
Chanzo: mwananchi.co.tz