Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya mafuta yapanda

8835 Mafuta+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mabadiliko haya ya bei yamechangiwa na kupanda kwa bei katika soko la dunia,

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) imetangaza kupanda kwa bei ya rejareja ya mafuta kwa Sh55 kwa lita moja ya petroli mwezi huu.

Tangazo la Ewura lililotolewa jana linaonyesha kupanda kwa viwango tofauti kwa bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Tangazo hilo linabainisha kuwa ongezeko la bei hizo limetokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia hivyo kuziathiri nchi zinazoagiza kutoka nje.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Ewura, Nzinyangwa Mchany alisema mabadiliko hayo ya bei yameanza jana nchini kote.

“Bei ya rejereja kwa mafuta yanayopita katika Bandari ya Dar es Salaam imepanda ikilinganishwa na ya mwezi uliopita,” alisema Mchany.

Wakati petroli ikipanda kwa Sh55 mwezi huu ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.4, dizeli imepanda kwa Sh19 sawa na asilimia 0.88 na mafuta ya taa Sh36 au asilimia 1.68.

Hata bei ya jumla nayo imepanda pia. Wauzaji wa nishati hiyo watanunua lita moja ya petroli kwa Sh54.85 zaidi kwa kila lita wakati dizeli ikipanda kwa Sh18.83 na mafuta ya taa Sh36.08.

“Mabadiliko haya ya bei yamechangiwa na kupanda kwa bei katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na bandari pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani inayotumika kwenye ununuzi wa nishati hiyo,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Taarifa ya Ewura inafafanua kuwa bei ya mafuta yanayopitia Bandari ya Tanga imepanda pia mwezi huu ikilinganishwa na iliyokuwapo Mei.

Inaeleza bei ya rejareja kwa Kanda ya Kaskazini imepanda kwa Sh9 kwa lita ya petroli na Sh39 kwa lita ya dizeli.

Kutokana na uchache wa mafuta yanayoingia kupitia Bandari ya Tanga, Ewura imewataka wauzaji kuagiza kutoka Dar es Salaam na bei yao itakokotolewa kwa kuzingatia umbali wa usafirishaji.

Kwa miaka kadhaa sasa, Ewura inatumia mfumo wa pamoja wa uagizaji mafuta kutoka nje (BPS) unaolenga kupunguza gharama ili kuwapa nafuu wananchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz