Kupanda kwa gharama za uzalishaji kumesababisha kupanda kwa bei ya kifaranga cha kuku kwa Sh300 kutoka Sh1, 800 hadi 2,100, hivyo kutishia mustakabali wa wafugaji.
Inaelezwa ongezeko hilo la bei lilianza kushuhudiwa tangu Juni, hali inayowaweka wafugaji katika wakati mgumu kiasi cha baadhi yao kufikiria kuacha kufuga.
Wakati wafugaji wakieleza hayo, kampuni za utotoleshaji vifaranga zinasema ongezeko la bei za nafaka na virutubisho vingine muhimu ni miongoni mwa sababu zilizochangia kupanda kwa bei ya vifaranga.
Bei ya nafaka zinazotumika kuandaa chakula cha vifaranga imeongezeka kati ya asilimia tisa hadi asilimia 49 katika miezi sita iliyopita, taarifa za Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaonyesha.
Gunia moja la mahindi la kilo 100 lililokuwa linauzwa kwa wastani wa Sh71,304 Mei sasa linapatikana kwa Sh106,305, wakati lile la mchele linauzwa Sh290,594 kutoka Sh213,125 na maharage nayo yakipanda kwa Sh97,471 na kuuzwa Sh296,000, huku gunia la mtama likipanda kwa Sh10,577 na kuuzwa Sh127,500.
Hata hivyo, Serikali imewataka wafugaji kutokata tamaa na kwamba bei ya nafaka ikishuka, vyakula vya kuku vitapungua, hivyo kushusha gharama za uzalishaji. Bei ya kifaranga imesema itafika Sh1,700.