Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya korosho sasa yawagawa wakulima

F08AF1DE 529A 45EC 8769 8582D9A4C493.jpeg Bei ya korosho sasa yawagawa wakulima

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakulima wa korosho wa vyama viwili vya ushirika vilivyoshiriki mnada wa pili wa uuzaji wa korosho jana mkoani Mtwara, walijikuta wakigawanyika katika uamuzi wa kuuza ama kutouza bidhaa hiyo kutokana na bei.

Wakati zaidi ya tani 10,046 zikiuzwa katika mnada huo wa pili ulioendeshwa na Chama Kikuu cha Masasi & Mtwara Cooperative Union (MAMCU), kilo 10,302,994 ziliingizwa sokoni na kuuzwa kwa bei ya juu Sh2,200 na bei ya chini ikiwa Sh1,800,

Hata hivyo, wakulima wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Newala na Tandahimba (Tanecu), wao waligomea kuuza korosho zao tani 2,045 katika mnada wao uliofanyika katika Kijiji cha Nanguruwe, Halmashauri ya Mji wa Newala.

Walilalamikia bei kuwa bado ni ndogo. Kilo moja kwa bei ya chini ilikuwa ikiuzwa kwa Sh1,800 na ya juu Sh2,200. Mnada huo ulikuwa ukifanyika katika Chama cha Msingi Kamundi Wilayani Nanyumbu.

Itakumbukwa, awali wakulima wa korosho katika mikoa miwili ya Mtwara na Lindi, mwishoni mwa wiki iliyopita walikataa kuuza zaidi ya tani 11,023 katika minada iliyofanyika Masasi na Tandahimba mkoani Mtwara na wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi.

Siku ya Alhamisi, wanachama wa Mamcu waligoma kuuza tani 6,513 za korosho ghafi baada ya wanunuzi kutoa kima cha chini cha bei ya kuanzia ya Sh1,800 na ya juu ya Sh2,200.

Juzi, vyama vya ushirika vya Ruangwa, Nachingwea na Liwale (Runali) vilitarajia kufanya mnada wa kwanza, lakini wa nne utafanyika katika mkoa unaolima korosho kwa msimu wa biashara wa 2022/23. Akizungumza katika mnada huo jana, Mwenyekiti wa MAMCU, Silaj Mtenguka alisema katika mnada huo, wanunuzi 20 walijitokeza na kununua korosho kwa bei ya juu ya Sh2,200 na ya chini ya Sh1,800.

“Katika mnada huu uliofanyika katika chama cha msingi Kamundi, kulijitokeza changamoto kidogo iliyosababishwa na watu wasio wakulima maarufu ‘kangomba’ kuingilia kati mnada, lakini tuliwadhibiti,” alisema Mtenguka.

Alisema kulikuwa na watu wasiokuwa wakulima, walitaka kuwalazimisha wakulima wakatae kuuza korosho yao lakini walishindwa.

Mtenguka alisema korosho hizo zimerudishwa mnadani baada ya kushindwa kuuzwa katika mnada wa kwanza uliofanyikia wilayani Masasi.

Akizungumza mnadani hapo, Bakari Nakanga, mkulima wa korosho Kijiji cha Nangaramo, alisema amelazimika kuuza korosho zake ili aweze kupata fedha za kumsaidia na familia yake.

Mkulima mwingine, Modesta Moses wa Kijiji cha Kamundi Wilaya ya Nanyumbu, alisema tangu mnada wa kwanza ulipofanyika, bei inakuja ileile, inaonyesha kuwa soko haliko vizuri mwaka huu.

“Mimi nimeuza, najua hali yangu, mahitaji yangu ni makubwa, nisipouza sasa sitaweza kumudu kuyatatua matatizo ya familia yangu, pia hata nikikataa kuuza, sijajipanga kubangua, sina uwezo wa kubangua nazipeleka wapi?” alisema.

Naye Bakari Mohamed, mkulima wa Kijiji cha Kamundi alisema kuwa amelazimika kuuza korosho hizo, baada ya kuona wanaopinga kuuza korosho hizo sio wakulima wa korosho na kusababisha sintofahamu kwa wakulima.

“Mimi ni mkulima, nalima navuna na kuuza, lakini kwenye biashara kuna matokeo mawili, kupata faida kubwa na kupata hasara, siwezi kupingana na soko la dunia na siwezi kuwa upande wa wauzaji wa kangomba ambao ndio wanaoghilibu wakulima ili wao wapate faida kubwa,” alisema Bakari.

Meneja Mkuu wa Tanecu, Mohamed Mwinguku aliliambia Mwananchi kuwa wakulima wamekataa kuuza korosho yao wakidai bado bei ni ndogo.

“Tulifikisha sokoni na tani 2,045 za korosho zimerudishwa ghalani,’’ alisema.

Chanzo: Mwananchi