Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya gesi yazidi kuvuruga wananchi

17b9ee59672ae7f348179718caf1ca4f Bei ya gesi yazidi kuvuruga wananchi

Tue, 10 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BEI ya gesi ya kupikia nchini imepanda kati ya Sh 2,000 hadi 4,000 na kuibua malalamiko kwa wananchi. Katika mikoa kadhaa gesi hiyo imeanza kupanda Agosti Mosi mwaka huu kwa mawakala wa jumla hadi rejereja.

Mkoani Kilimanjaro, wauzaji na wasambazaji wakubwa wa gesi wameeleza hofu yao kuhusu biashara ya gesi ya kupikia nyumbani kuyumba baada ya kupanda kwa bei.

Wanasema, bei imepanda kutoka Sh 50,000 hadi Sh 54,000 kwa mtungi wa kilo 15 huku mtungi wa kilo sita uliokuwa ukiuzwa Sh 21,000 sasa unauzwa Sh 23,000.

Hii ni mara ya pili bei ya gesi inapanda kufuatia kupanda kwa bei ya gesi katika soko la dunia ambako pia huambatana na kupanda kwa bei ya mafuta. Februari 2020, bei ya gesi nchini iliwahi kupanda kati ya Sh 3,000 na 5,000 pia.

Wananchi wamesema, kupanda kwa bei ya gesi ghafla ni kuendelea kuwaumiza wananchi wa hali ya chini na hivyo wakaiomba Serikali kuingilia kati kupunguza bei hiyo.

Kufuatia kupanda kwa bei, mtungi wa Oryx wa kilo 15 ulikuwa umeanza kuuzwa Sh 54,000 kutoka Sh 52,000, mtungi wa kilo sita, uliuzwa kwa Sh 23,000 kutoka Sh 21,000 na wa kilo 38 ulibaki Sh 125,000 za zamani.

Morogoro baadhi ya mawakala wa gesi walisema bei iliyopo ni ya zaidi ya miezi mitatu ambapo wanauza sh Sh 48,000 hadi 50,000 kulingana na eneo na ununuzi wake.

Huko Serengeti mkoani Mara, mtungi wenye ujazo wa kilogramu 15 uliripotiwa kuuzwa kwa bei ya kati ya Sh 52, 000 hadi Sh 53, 000. Awali ilikuwa Sh 50, 000.

Jijini Mwanza, mtungi wenye ujazo wa kilo sita uliokuwa ukiuzwa kati ya Sh19, 000 hadi Sh21,000 sasa unauzwa kati ya Sh22, 000 hadi Sh23, 000 na huko mjini Sengerema ilipanda kutoka Sh19, 000 hadi Sh21,000.

Hata hivyo, jijini Dodoma, makao makuu ya serikali, imeripotiwa hakukuwa na mabadiliko ya bei ambapo mtungi wa kilo sita unauzwa kwa Sh 40,000 ukiwa mpya na bei ya kujaza Sh 21,000 ambayo ni bei ya siku zote.

Mkuu wa idara ya Biashara na Usambazaji Oryx Gas Tanzania, Mohamed Mohamed anasema bei ilipanda katika soko la dunia tangu Mei mwaka huu kutoka dola za Marekani 475 kwa tani hadi dola 525 za Marekani Juni, dola 620 za Marekani Julai kabla ya kupanda hadi dola 655 Agosti.

Mohammed anasema bei ya gesi imekua isiyotetereka kwa muda mrefu lakini katika miaka saba iliyopita imekua ikiongezeka na hadi sasa inaendelea kuongezeka.

Anasema, kwa kawaida kwenye soko la dunia bei za gesi zinaongezeka kuanzia Novemba hadi Februari kipindi ambacho watu wa kanda za kaskazini za dunia hutumia gesi kama suluhisho la kupambana na kipindi cha baridi.

Kufuatia kupanda holela kwa bei hiyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji, (Ewura) ilisitisha bei hiyo na kuonya wafanyabiashara watakaoendelea kupandisha.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo anasema taarifa walizonazo ni kampuni moja tu ya Oryx iliyoandika barua kuomba kupandisha bei kutokana na madai ya kupanda bei ya gesi katika soko la dunia.

Anasema Ewura inafuatilia suala hili kujua bei halisi katika soko la dunia na taarifa rasmi zitatolewa. Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wamedai bei ya gesi imepanda kutokana na wao kununua kwa bei kubwa kutokana na bei ya gesi katika soko la dunia kupanda.

“Ewura imesitisha ongezeko jipya la bei za gesi nchini hadi tutakapopokea sababu za msingi za kuongeza bei na kuzithibitisha kuwa zina mashiko,” Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Godfrey Chibulunje naye alikariwa akisema.

Kwa mujibu wa taarifa za jarida la Ewura, matumizi ya gesi ya kupikia nyumbani yaliongezeka kwa asilimia 33,

mwaka 2018 ikilinganishwa na matumizi hayo 2017.

Kuongezeka huko kumetokana na juhudi za serikali kutoa

elimu kwa umma juu ya faida za matumizi ya gesi

dhidi ya matumizi ya mkaa na mafuta ya taa.

Jarida hilo lilimkariri Kaguo akisema, ongezeko hilo limetokana na wananchi wengi kuelewa umuhimu na unafuu wa gesi ya kupikia ukilinganisha na nishati nyingine ili kuendana na sera ya taifa ya nishati (NEP) ya mwaka 2015 inayosisitiza matumizi ya

nishati mbadala ili kuboresha maisha ya wananchi.

Anasema, uagizaji wa gesi uliongezeka hadi kufikia

tani 142,940 mwaka 2018, ongezeko la asilimia 33 ikilinganishwa na tani 107, 263 zilizoingizwa nchini kwa mwaka 2017.

Kaguo anasema, haya ni mabadiliko makubwa katika matumizi ya gesi, hasa ikizingatiwa mwaka 2010 matumizi yake yalikuwa tani 20,000 tu.

Anasema, pamoja na ongezeko la utumiaji wa gesi ya

kupikia, bado maeneo mengi ya vijijini nishati hiyo haipatikani au wasambazaji wake ni wachache, hivyo wananchi wa maeneo hayo wanaendelea na matumizi ya kuni, mkaa na mafuta ya taa vinavyohatarisha mazingira.

Kuhusu haki za watumiaji gesi kufuatia kupanda kwa bei ya gesi au upungufu wa ujazo wa mtungi, Kaguo anasema katika jarida hilo kuwa, “Kila muuzaji wa gesi ya kupikia majumbani lazima awe na mzani wa kupima mtungi na uzito wa gesi na mtungi lazima uwe kama ulivyoandikwa katika mtungi, pia mtungi ni lazima uwe na lakiri.”

Kaguo anasisitiza wananchi kusoma mkataba wa Ewura wa huduma kwa mteja ambao umeandikwa katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza ukielezea wajibu wa Ewura, mteja na mtoa huduma ili wapate haki zao.

Nishati mbadala kama gesi ya kupikia au umeme imeelezwa kuwa ni chanzo chochote cha nishati ambacho ni mbadala kwa mafuta ya visukuku. Ni nishati ambazo hazikaushi rasilimali za dunia na hazichafui mazingira.

Nishati hizi mbadala zinalenga kushughulikia wasiwasi kuhusu nishati ya visukuku, kama vile utoaji wake wa viwango vikubwa vya gesi ya ukaa ambayo inachangia sana kuongezeka kwa joto la dunia. Nishati ya majini, umeme utokanao na maji, upepo, joto la ardhini, gesi na mwanga wa jua vyote hivi ni vyanzo vya nishati mbadala.

Kwa mujibu wa DW, wanasayansi 14,000 wamehimiza juu ya dharura ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ulimwenguni. wanasanyasi hao wamesema uchumi wa dunia umeathiri kwa kiwango kikubwa uhai na dunia.

Hivyo, kupanda kwa bei ya gesi huenda kuathiri sana juhudi za kuhifadhi mazingira nchini kwani kunamaanisha watu kuendelea kutumia nishati za kuni wakati miti ni kitu muhimu katika mazingira yetu yanayo tuzunguka. Ni chanzo kikubwa cha maji na pia hunyima hewa ukaa. Miti ndiyo kila kitu hivyo jamii inashauriwa kutunza vyema mazingira kwa kutumia nishati mbadala kama gesi ya kupikia.

Jamii ijue ikikata miti ovyo itasababisha majanga kama kukosa vyanzo vya maji na mmomonyoko wa udongo. Mazingira yaliyozungukwa na viwanda yanatishia amani kwa jamii yetu nchini hasa kwa watu wanaoishi katika maeneo haya yanayozungukwa na viwanda. Watu waishio katika mazingira haya wanapata tabu kutokana na moshi.

Zaidi ya asilimia 90 ya wakazi Kusini mwa Jangwa la Sahara inategemea ama kuni au mkaa. Nishati ya miti huchangia yapata asilimia 90 ya nishati ya kupikia nchini Tanzania. Mkaa unatumika zaidi mijini wakati kuni hutumika zaidi vijijini. Asilimia 70 ya kaya za mijini hutegemea mkaa.

Afrika huzalisha asilimia 62 ya mkaa wote duniani ambao unakisiwa kufikia tani milioni 52. Tanzania inashika nafasi ya saba kwa uzalishaji wa mkaa duniani, ikichangia kama asilimia 3 ya uzalishaji wa mkaa wote duniani, kwa kiasi cha zaidi ya tani 1.6. Mkaa huchangia zaidi ya Dola za Marekani milioni 2.7 (Sh bilioni 6.2 za Tanzania) kwa mwaka kwenye uchumi wa Tanzania na ni chanzo kikubwa cha ajira na kipato cha watu mijini na vijijini.

Ili kuhakikisha nishati ya miti inakuwa endelevu, iko haja kuwepo uzalishaji endelevu wa miti kupitia misitu endelevu na usimamizi shirikishi wa misitu. Badhi ya mikoa kama Morogoro inaendesha uzalishaji wa mkaa kwa njia endelevu, mpango ambao umeonekana kulinda mazingira kuliko mkaa mwingi nchini unaozalishwa kwa njia holela.

Iko haja kwa jamii kuachana na matanuru asilia ya kuchomea mkaa na kutumia matanuru ya kisasa yenye ufanisi zaidi kama inavyofanyika kwenye miradi ya mkaa endelevu mkoani Morogoro kupitia Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (CoFCorEST).

Inashauriwa pia wananchi kuachana na majiko asilia na kutumia majiko ya kisasa na hivyo kupunguza hewa ya ukaa kwa asilimia 80.

Chanzo: www.habarileo.co.tz