Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya Vanilla yashuka zaidi

Vanilla Pemba Bei ya Vanilla yashuka zaidi

Tue, 14 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima wa Vanilla kisiwani Pemba wamelalamikia kushuka kwa bei ya zao hilo kutoka shilingi milioni moja kwa kilo hadi shilingi 400,000

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kongamano la kilimo cha viungo lililofanyika kisiwani Pemba, wakulima hao walisema wanunuzi wa zao hilo wanadai kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 umechangia kushuka kwa bei ya zao hilo.

Muhammed Ali Mmanga kutoka Kijiji cha Daya Mtabwe Pemba, alisema kuwa kabla ya ugonjwa wa UVIKO-19 walikuwa wakiuza kilo moja ya vanila Sh. 1,000,000, lakini kwa sasa wanauza Sh. 400,000.

Alisema kuwa bei ya Sh. 400,000 kwa kilo moja ya zao hiyo ni hasara kubwa kwao kutokana na ugumu wa kilimo hicho. “Mimi binafsi kwa sasa nimeamua kufungia ndani vanila nilizonazo kwa sababu bei ya sasa ni hasara kubwa kwangu,” alisema.

Aliiomba serikali kuweka utaratibu wa kulinunua zao hilo ambalo lina thamani kubwa kama inavyonunua zao la karafuu.

Alieleza kuwa endapo serikali itaamua kulinunua zao hilo la vanila na mazao mengine ya viungo, wafanyabiashara wataacha kuwalangua wakulima kwa kuweka bei watakazo wao kwa maslahi yao binafsi.

“Tunapowapelekea wanunuzi wetu kununua vanila wanasema kuwa kutokana na UVIKO-19 bei ya vanila imeshuka duniani sasa sijui kama ni kweli au corona imekuwa kama ni kichaka na kutaka kutukandamiza,” alisema.

Baraka Masoud Kasezero kutoka Taasisi ya viungo Tanzania (TASPA’), alisema kuwa ushuru ni mkubwa katika kusafirisha bidhaa za viungo ikiwamo vanila hasa ikizingatiwa kuwa soko kubwa la bidhaa za viungo lipo nje ya nchi hasa Bara la Ulaya.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu Zanzibar, Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema kuwa serikali haipangi bei ya mazao bali hutokana na soko la dunia lilivyo.

“Hivi karibuni tulikuwa na wasiwasi kuhusu bei ya karafuu kutokana na corona, lakini tunashukuru soko la dunia halikushuka, hivyo kwa upande wa vanila kama bei imeshuka itabidi tuangalie je, kushuka bei kunasababishwa na soko la dunia au wafanyabiashara wanawaumiza wakulima,” alisema.

Alieleza kuwa kuhusu kushuka kwa bei ya zao la vanila serikali yake italifanyia kazi ili kuangalia soko la dunia likoje kuhusu vanila na kama litakuwa limeanguka, hakuna njia lazima kukubaliana na hali hiyo.

Tanzania ina aina 30 ya viungo vinavyotumia kilimo hai ikiwamo vanila, karafuu, pilipili manga, tangawizi, pilipili kichaa, mdalasini, iliki, mchaichai na vingine ambavyo hutumika kwa chakula na dawa.

Kaya 1,050 Tanzania zinatarajiwa kufaidika na mradi wa kilimo hai cha mazao ya biashara ya viungo kupitia mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambao unawasaidia wakulima kuwatafutia masoko ya mazao hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live