Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya Saruji ni maumivu tu

Saruji Pc Data Saruji

Wed, 27 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya uzalishaji wa saruji kuwa zaidi ya mahitaji ya nchi, bei imeendelea kuwa juu, huku gharama za uzalishaji zikitajwa kuwa chanzo.

Kwa mujibu wa Serikali, uzalishaji wa saruji nchini umefikia tani milioni 11 kwa mwaka, huku mahitaji ya nchi yakiwa ni tani milioni 7.5 kwa mwaka.

Ongezeko hilo la uzalishaji limewafanya wanunuzi watarajie kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo madukani, kama ilivyozoeleka katika bidhaa nyingine.

Hata hivyo, bei ya mfuko mmoja wa kilogramu 50 wa saruji imebaki kuwa Sh17,000 hadi Sh19,000 kwa muda mrefu wakati wazalishaji wakiendelea kusaka masoko ya nje ya nchi.

Wazalishaji wanasema wasingeweza kupunguza bei ya bidhaa hiyo, ilhali gharama za uzalishaji wake zimeongezeka kama ilivyofafanuliwa na Meneja wa Masoko wa Tanzania Portland Cement PLC, inayozalisha Twiga Cement, Danford Semwenda.

Alisema wazalishaji wa saruji wanatumia fedha nyingi kwenye uzalishaji na ndizo zinazochagiza bei ya bidhaa hiyo isalie kama ilivyo sasa ili kuepuka hasara.

“Tunatumia fedha nyingi kuzalisha na ndiyo maana bei inakuwa kubwa nchini. Kama ilivyo katika bidhaa nyingine, bei ya saruji inaongezeka na kupungua kulingana na gharama za uzalishaji,” alisema Semwenda.

Alisema kuingizwa kwa vipuri kutoka nje ya nchi vinavyotumika kuzalisha bidhaa hiyo, ndiyo moja ya sababu ya ongezeko la gharama za uzalishaji nchini.

“Katika kipindi hiki wafanyabiashara wanakabiliwa na uhaba wa dola, ni changamoto kubwa, hasa kwa wazalishaji wa saruji kwa sababu tunauza kwa shilingi wakati vipuri tunanunua kwa dola. Ukweli hii ni changamoto kubwa,” alisema Semwenda.

Kukosekana kwa umeme wa uhakika ni sababu nyingine iliyotajwa na Semwenda ya kuongeza gharama za uzalishaji.

Alisema wazalishaji wanalazimika kuwa na vyanzo mbadala vya nishati ambavyo kimsingi ni ghali.

“Tuna changamoto ya umeme nchini na wazalishaji wanazalisha muda mwingi. Ndiyo maana uzalishaji unaonekana kuwa na gharama kubwa. Kutumia vyanzo mbadala ni gharama, inaweza kuwa mara mbili au tatu ukilinganisha na umeme wa kawaida,” alisema.

Alisema hakuna kampuni inayolenga kuwekeza ili ipate hasara, hivyo bei ya sasa ya saruji inaendana na gharama za uzalishaji.

Mkurugenzi wa Sera na Uchechemuzi wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Akida Mnyenyelwa alisema hali hiyo inawafanya wazalishaji wapange bei itakayowapa faida.

“Kuna haja ya kutatua changamoto inayoongeza gharama za uzalishaji ili kupunguza bei ya saruji,” alisema Mnyenyelwa.

Alisema kwa kufanya hivyo, Tanzania itajiwekea ushindani mzuri katika Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) kwa sababu saruji inayozalishwa ni bora, kinachokwamisha masoko ni bei.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alisema Serikali ilijadiliana na wamiliki wa viwanda vya saruji hivi karibuni na wanapaswa kutafuta namna ya kutumia fursa ya AfCFTA.

Alisema wazalishaji waliweka wazi kuwa gharama za uzalishaji wa saruji nchini ndiyo sababu ya kuongezeka kwa bei ya bidhaa hiyo dukani.

“Tumeanza kufanyia kazi mambo yote hayo, kwa sababu saruji yetu ni ghali na ndiyo maana tunapata changamoto kulifikia soko la Afrika,” alisema Dk Kijaji.

“Haitachukua muda tutatambulisha bidhaa zetu AfCFTA, kwa sababu tunazalisha zaidi. Hivyo hata ikiuzwa katika mataifa mengine hakutakuwa na uhaba nchini. Pia ni sehemu ya kuinua maendeleo ya kiuchumi.”

Alisema bei ya bidhaa hiyo itaanza kupungua nchini kwa kadiri changamoto zilizopo zitakavyoendelea kutatuliwa, lakini hakuweka wazi ni lini hasa hilo litatekelezwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live