Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Mkoa wa Ruvuma umepangiwa makampuni matano ya kusambaza mbolea, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutoa ruzuku ya shilingi 150 bilioni ili kushusha bei ya mfuko wa bidhaa hiyo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akiongea na Wanakijiji wa Migelegele baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo, mkoani humo hii leo Oktoba 18, 2022.
Amesema, “Makampuni matano ya Mohammed Enterprises, Yara, OCIP, Premium na ETG yamepangiwa kuleta mbolea hapa mkoani, na hadi sasa tayari tani za mbolea 9,000 zimeshawasili na kati ya hizo, tani 2,467 zimeshaenda vijijini.”
Majaliwa ameendelea kubainisha kuwa, “Mahitaji ya mkoa mzima ni tani 67,000 kwa hiyo hizi tani 9,000 hazitoshi. Watu wa TFL simamieni ili iletwe haraka. Mbolea za kupandia zije sasa na za kukuzia zije baadaye. Jitahidini kuongeza idadi ya mawakala ili wananchi wafikiwe huko waliko.”