Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei ya Mafuta ya Kula yapaa katika soko la dunia

MAFUTA 112 Imeelezwa kwamba nchi inapitia mfumuko kutokana na bidhaa zinazoingia kupanda

Tue, 17 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametoa hotuba Bungeni leo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo 2022/2023 ambapo amesema "Bei ya mafuta ya kula katika soko la dunia imepanda kutoka Dola za Marekani 1,631 Machi, 2021 hadi Dola za Marekani 2,250 Machi, 2022 sawa na ongezeko la 38%, Dunia inaendelea kupitia changamoto ya vita kati ya Ukraine na Urusi na athari za UVIKO-19 ambazo zimeleta mabadiliko ya mifumo ya ugavi na gharama za usafirishaji za bidhaa na huduma kimataifa katika uchumi wa dunia"

"Hali hiyo, imesababisha nchi kukabiliwa na mfumuko wa bei unaoingia (Imported inflation) kutokana na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hali inayoathiri ustawi wa wananchi, aidha athari za UVIKO-19 na mgogoro unaoendelea kati ya Ukraine na Urusi kutokana na tafiti mbalimbali za kimataifa utaathiri mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali"

"Wizara imeendelea kutekeleza malengo ya Serikali ya kuondoa utegemezi wa mazao na bidhaa za kilimo zenye uhitaji mkubwa ambazo huagizwa nje ya nchi kama vile mafuta ya kula, ngano na sukari, Wizara imesambaza kwa wakulima tani 2,000 za mbegu za alizeti kwa ruzuku ya Shilingi Bilioni 5.84, mbegu hizo zimesambazwa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Manyara kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula"

"Aidha, mbegu hizo zitatoa mavuno ya mbegu za alizeti ya kukamua tani 400,000 ambazo zitazalisha mafuta ya kula tani 100,000, sambamba na zao la alizeti, Wizara imeendelea kutekeleza mpango wa muda mrefu wa kuzalisha miche bora ya chikichi na kuigawa bure kwa wakulima ambapo jumla ya miche 896,029 imesambazwa katika mikoa ya Kigoma, Mbeya, Mtwara, Kagera, Tanga na Katavi"

Chanzo: www.tanzaniaweb.live