Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei vifaa vya ujenzi pasua kichwa!

Vifaa Ujenzi Bei vifaa vya ujenzi pasua kichwa!

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bei ya vifaa vya ujenzi imeendelea kupanda maeneo tofauti nchini kwa miezi sita mfululizo, jambo lililowafanya baadhi ya wananchi kusitisha ujenzi huku wafanyabiashara wakilia kutopata wateja.

Vifaa ambavyo bei zake zimepaa zaidi ni nondo, mabati na saruji. Katika baadhi ya maeneo, bidhaa za kuwekea dari mfano gypsum na za chuma ikiwamo misumari na nyaya zimepaa pia.

Bei hizo zilianza kupanda Septemba mwaka jana sababu kubwa ikitajwa ni kupanda kwa bei kwenye soko la dunia hasa chuma kinachotoka China ambaye ni muuzaji mkubwa zaidi n chini.

Uchunguzi wa Serikali umebaini ongezeko la gharama kwenye bidhaa za chuma ulisababishwa na kupanda kwa bei za malighafi na kwa saruji, hakukuwa na ongezeko lolote, hivyo ilionya juu ya wote wanaopandisha bei ya saruji kiholela.

Licha ya Waziri wa Viwanda na Biashara mpaka Januari, Profesa Kitila Mkumbo kuwaonya wanaopandisha bei ya saruji Novemba mwaka jana, imeendelea kuwa juu kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumzia mikakati iliyopo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema wizara inafanya uchambuzi kujua tatizo liko kwa wazalishaji au wasafirishaji. Hata hivyo, alisema wamebaini gharama hazijapanda sana licha ya changamoto za malighafi hasa za chuma.

“Baada ya hapo Waziri (Dk Ashatu Kijaji) atakuja kutoa statement (taarifa) kujua nini hasa lakini pia tunajaribu kuona kama kuna watu wanapandisha bila sababu Serikali tudhibiti. Mheshimiwa Waziri atakutana na wasafirishaji kujua shida inayosababisha kuongezeka kwa bei na mambo mengine,” alisema Kigahe.

Kigahe aliongeza kuwa Serikali imeiagiza pia Tume ya Ushindani (FCC) kufanya uchunguzi ili kujua kinachosababisha ongezeko hilo la bei.

Hata hivyo, wenye viwanda vya bidhaa za chuma wamesema ongezeko la bei kwenye mabati na nondo kumesababishwa na kupanda kwa malighafi kwenye soko la dunia hivyo ni jambo lililo nje ya uwezo wao.

Meneja wa kiwanda kinachozalisha bidhaa za chuma cha MMI Steel, Heramb Kumthekar alisema hutoa malighafi China, Japan na India ambako bei imepanda.

“Hatuwezi kufanya chochote kuondoa tatizo hili kwa sababu siyo sisi tunaoamua bei, tunakwenda kununua malighafi tu, kwa hiyo liko nje ya uwezo wetu,” alisema Kumthekar.

Meneja mauzo wa Kampuni ya Twiga Cement, Danford Semenda alisema: “Sorry (samahani) sisi hatujapandisha bei miaka miwili iliyopita.”

Mafundi upauaji waeleza

Wakizungumza na Mwananchi, mafundi upauzi walisema mbao zimepanda bei kiasi cha wengi kuzikimbilia za mlingoti ambazo zilizopanda kutoka Sh8,000 hadi Sh12,000 kwa futi.

“Tukienda wanatueleza ushuru umekuwa mwingi huko barabarani na ukiangalia mlingoti unatoka mikoa ya Ruvuma na Iringa ambako kwa tani moja walikuwa wanatozwa Sh27,000 lakini imepanda hadi kati ya Sh45,000 na Sh50,000 na vituo wanavyosimamishwa ni vingi,” alisema Jofrey Mkiza, fundi mwenye ofisi Mtaa wa Mabibo.

Ally Kidimo wa mtaa huo pia alisema huchukulia mbao Manzese ambazo ni za mkongo, mtondoo, mninga, mvule, mpilipili na msegerea ambazo ni nzuri lakini za futi 12 zimepanda kutoka Sh35,000 hadi Sh70,000.

“Kutokana na soko la bidhaa hiyo kuwa huria watu wamekuwa wakikimbilia kwenye bidhaa za chuma ambazo hata hivyo zimepanda kwa kiasi kikubwa japo mbao zinaonekana kupaa zaidi,” alisema fundi Kidimo.

Hali ilivyo Arusha

Mfanyabiashara wa jumla mkoani hapa, Reginald Masawe alisema bei ya chuma na bati ndio zimepanda zaidi zikiongezeka kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000.

“Mfano chuma cha milimita 10 kimepanda kutoka Sh16,500 hadi Sh20,000, bei ya mabati imepanda kwa kati ya Sh3,000 hadi Sh10,000 huku ya rangi ikiongezeka kwa Sh5000,” alisema.

Hata hivyo, bei ya saruji mkoani Arusha imepungua kwa kati ya Sh1,000 hadi Sh3,000 kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kwa sababu ya kufunguliwa kwa kiwanda kipya cha saruji cha Huwaxi kinachomilikiwa na Wachina huko mkoani Tanga.

Mwanza na Musoma

Jijini Mwanza, bei ya saruji aina ya Twiga imepanda kutoka Sh20,000 hadi Sh22,500 huku ile ya Dangote ikitoka Sh19,000 hadi Sh21,000 na nondo za milimita 12 zikitoka Sh25,000 hadi Sh27,000 siku za hivi karibuni.

Tripu moja ya lori la mchanga unaotolewa ziwani nayo imepanda kutoka Sh60,000 hadi Sh100,000 kutegemea na eneo aliko mteja.

Mkazi wa Mtaa wa Tambukareli jijini hapa, Haruna Msekwa alisema mwaka jana alinunua tripu moja ya mchanga kwa Sh60,000 lakini ilipanda mpaka Sh80,000 na sasa ni Sh100,000.

“Hebu fikiria hapa Tambukareli sio mbali sana na Ziwa Victoria, kwa nini bei ya mchanga ipande kiasi hicho? Matofali sasa yanauzwa kati ya Sh1,200 hadi Sh1,500 ukilinganisha na bei ya awali ya Sh1,000, tunaweza kusema ni kutokana na kupanda kwa bei ya saruji, sasa bei ya mchanga imepandishwa na nini?” aliendelea kuhoji Msekwa.

Mfuko wa saruji uliokuwa ukiuzwa Sh18,500 sasa umepanda hadi kati ya Sh21,000 na Sh22,000 wakati nondo ya milimita 12 iliyokuwa ikiuzwa Sh18,000 sasa ni kati ya Sh27,000 hadi Sh28,000 huku ya milimita 16 iliyokuwa inauzwa Sh37,000 sasa ni Sh50,000.

Bei ya vifaa vya ujenzi mjini Musoma inazidi kupanda kwani awali mfuko mmoja wa saruji ulikuwa ukiuzwa kati ya Sh20,000 hadi Sh21,000 lakini sasa ni kati ya Sh24,000 hadi Sh25,000.

Ongezeko hilo la bei linahusishwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa kutokana na mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kukabili athari za Uviko-19 kulikoongeza mahitaji sokoni.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi wakati akikagua ujenzi wa madarasa katika wilaya hiyo, nondo iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh23,000 ilipanda hadi kufikia Sh28,000.

Dar es Salaam

Hali haiko tofauti jijini hapa ambako saruji inauzwa kati ya Sh15,500 hadi Sh17,500 huku mabati yakigharimu kati ya Sh24,000 na Sh27,000 kulingana na maeneo.

Makali ya bei pia yameonekana kwenye nondo ambazo huko nyuma zilikuwa zikiuzwa Sh23,000 sasa zimefikia Sh27,000.

Upande wa gypsum board zinauzwa kati ya Sh23,000 hadi Sh25,000 kulingana na tofauti ya maeneo huku ikibainishwa kuwa bei hizi zinachangiwa na gharama za usafirishaji.

Akizungumza na Mwananchi, Abdallah Juma ambaye ni fundi ujenzi alisema kuendelea kupanda kwa bei za vifaa hivyo kunasababisha watu kusimamisha ujenzi hivyo wao kukosa kazi kwa muda huu.

“Maisha yetu mafundi yanategemea mtu ajenge sasa kama hakuna ujenzi tunapitia wakati mgumu, ukweli ni kwamba Januari hii watu hawajengi. Sababu kubwa ni ukata lakini vifaa navyo viko juu sana, mtu ukimpa orodha ya vifaa vinavyohitajika akaenda dukani, akapiga hesabu zake anaona bora asogeze mbele shughuli hiyo,” alisema Juma.

Dodoma

Mfanyabiashara katika Koko la Majengo, Issa Rehemu alisema kwa sasa mabati ya kawaida ya geji 30 yamepanda kutoka Sh19,000 hadi Sh23,000.

Alisema bati za rangi zimepanda kutoka bei ya awali ya Sh27,000 hadi Sh29,000 kwa geji 30 huku zenye geji 32 zikipanda kutoka Sh23,000 hadi Sh27,000.

“Kwa miezi iliyopita bei za vifaa vingi ilipanda mpaka sasa kuna vingine vimepanda zaidi, kifupi bado hali ya bei haieleweki,” alisema.

Kigoma

Bidhaa za ujenzi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji zimepanda ikilinganishwa na miezi miwili nyuma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wauzaji wa bidhaa hizo walisema zilizopanda ni saruji, nondo, mabati, mbao, rangi na marumaru.

Mfanyabiasha Amon Nyete alisema nondo ya milimita 10 ilikuwa Sh21,000 lakini imepanda hadi Sh25,000 na ya milimita 12, awali ilikuwa Sh24,000 ila sasa ni Sh28,000.

Bati za rangi alisema bandari moja ilikuwa Sh432,000 zikapatanda hadi Sh470,000 jambo ambalo sio kawaida kwa hapo awali.

Muuzaji Hilda Samweli, alisema kopo la rangi la lita nne walikuwa wanauza Sh20,000 lakini imepanda hadi Sh23,000 na ndoo ya lita 20 walizokuwa wanauza Sh38,000 imefika Sh40,000 wakati marumaru ya sentimita 50 kwa 50 waliyokuwa wanauza Sh50,000 imefika Sh 55,000.

Imeandikwa na Peter Elias na Elizabeth Edward (Dar), Mussa Juma, Saada Amir (Mwanza), Beldina Nyakeke (Musoma) na Suzy Butondo (Shinyanga), Mainda Mhando (Dodoma) na Happiness Tesha (Kigoma).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live