Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bei mafuta ya petroli, dizeli yapanda Tanzania

74143 Mafuta+pic

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) nchini Tanzania imetangaza bei za kikomo kwa bidhaa za mafuta nchini humo zitakazoanza kutumika kuanzia kesho Jumatano Septemba 4,2019.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Septemba 3,2019 kwa vyombo vya habari na mkuu wa kitengo wa mawasiliano na uhusiano kwa umma wa Ewura, Wilfred Mwakalosi amesema bei za jumla na rejareja za mafuta za petroli dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka.

Mwakalosi amesema mafuta hayo ni yale yaliyoingia kupitia bandari ya Dar es Salaam ambayo yameongezeka ukilinganisha na mwezi uliopita.

“Mwezi huu (Septemba) bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa Sh83 kwa lita (sawa na asilimia 3.87), Sh61 kwa lita (sawa na asilimia 2.90), Sh46 kwa lita (sawa na asilimia 2.22),” amesema

Amesema bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na yanayoingizwa kupitia bandari ya Tanga yameongezeka ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.

“Kwa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara mwezi huu bei zimeongezeka kwa Sh108 kwa lita sawa na asilimia 4.95 na  Sh72 (sawa na asilimia 3,36),” amesema Mwakalosi.

Pia Soma

Advertisement   ?
Katika taarifa hiyo, Mwakalosi amesisitiza bei ya mafuta ya taa kwa mikoa ya kaskazini zitaendelea kutumika zile zilizochapishwa mwezi uliopita kwa sababu hakuna shehena ya bidhaa hiyo iliyoingia kupitia bandari ya Tanga.

Mbali na hilo, Mwakalosi amesema bei za jumla na rejareja ya mafuta petroli na dizeli yaliyoingizwa kupitia bandari ya Mtwara zimeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Amesema bei za rejareja za petroli na dizeli kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma zimeongezeka kwa Sh99.09 kwa lita (sawa na a silimia 4.73) na Sh61.41 (sawa na asilimia 3.02).

“Kwa kuwa hakuna mafuta ya Taa yaliyopokelewa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta ya kusini wanashauriwa kununua mafuta haya Dar es Salaam,” amesema.

Amefafanua bei ya rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na kusafirishwa kwenye mkoa husika.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz