Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa wazawa wa Kagera wanaoishi nje ya mkoa pamoja na nje ya nchi (Diaspora) kuwekeza mkoani humo kwani Serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa barabara.
Ametoa wito huo leo katika ibada ya Krismasi katika Parokia ya Bikira Maria Mbarikiwa Bushangaro - Nyakaiga, Karagwe mkoani Kagera ambapo amewapongeza Wanakagera wanaoendelea kuwekeza katika mkoa huo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kumuunga mkono na kumuombea afya njema Rais Samia Suluhu Hassan ili azidi kutenda kazi yake ya kuleta maendeleo ambapo amesema kazi ya kuwahudumia wananchi ni ngumu hivyo inahitaji maombi ambayo yatamlinda na kumsaidia kuzidi kuwa na hekima na busara katika uongozi wake.
Katika Mahubiri, Padri Georges Kimonge amekemea tabia ya vijana kujihusisha na matendo yasiyompendeza Mungu hususan suala la kutoa mimba ambapo amesema si jambo zuri kuua kiumbe ambacho Mwenyezi Mungu amepanga kukileta duniani kwa sababu maalum.