Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashungwa awaita wenye viwanda vilivyofungwa wizarani

Wed, 2 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma.  Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa ameagiza wamiliki wa viwanda vya samaki katika mikoa ya kanda ya ziwa ambavyo vinafanya kazi kwa kusuasua na vilivyoacha uzalishaji wafike wizarani mara moja ili waweze kujadiliana namna ya kutatua changamoto hizo.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo leo Jumanne Oktoba 1, 2019 mjini Musoma mkoani Mara baada ya kukagua kiwanda cha samaki cha Prime  Catch ambacho kimesimamisha uzalishaji kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Amesema serikali haiwezi kufikia sera yake ya uchumi wa viwanda endapo viwanda hivyo vya samaki vyenye mchango mkubwa katika uchumi wa mikoa  ya kanda ya ziwa na Taifa kwa ujumla vitaendelea kufanya kazi kwa kusuasua au kufungwa kabisa.

Bashungwa amesema umefika wakati wamiliki wa viwanda hivyo kukutana na wizara husika ili kujadili kwa  pamoja juu ya changamoto hizo ili kuweza kupata suluhisho la kudumu na hatimaye viwanda hivyo viweze kufanya kazi kwa uhakika zaidi.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kiwanda kilichoanzishwa kinafanya kazi.

"Nitoe wito kwa wamiliki wote waje wizarani tukae tuanze kupitia kiwanda kimoja baada ya kingine, tujue shida iko wapi na nini kifanyike ili uzalishaji uweze kufanyika kama ilivyo kusudiwa badala ya majengo  kuwepo tu huku  hakuna kitu kinafanyika," amesema Bashungwa

Pia, waziri huyo amewaagiza makatibu wakuu wa wizaraa ya biashara pamoja na wizara ya mifugo na uvuvi kuandaa mkutano wa  pamoja utakaoshirikisha wadau wa sekta ya viwanda na uvuvi mkoani Mara ili kuweza kujadili namna  ambavyo  sekta hizo zinaweza kufanya kazi pamoja na kufanikisha lengo la uchumi wa viwanda.

Awali, Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima aliomba wizara ya viwanda pamoja na ofisi ya mwanasheria mkuu a serikali kuingilia kati suala la umiliki wa kiwanda cha Prime Catch ambacho kiliacha uzalishaji mrefu huku wamiliki wake wakiwa hawapo tayari kutoa hati za kiwanja ambapo kiwanda hicho kilijengwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz