Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashungwa atangaza ukomo bei ya barakoa

BASH.webp Bashungwa atangaza ukomo bei ya barakoa

Tue, 28 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, amesema atachukua hatua kwa taasisi zisizo za kiserikali (NGO) zinazouza barakoa kwa gharama kubwa.

Bashungwa alitoa tahadhari hiyo mkoani Arusha, alipotembelea viwanda vya kuzalisha nguo vya Sunflug na A to Z kuangalia hali ya uzalishaji wa barakoa katika viwanda hivyo.

Bashungwa alitoa onyo kwa NGO zilizoomba kibali cha kuzalisha barakoa kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania lakini badala yake wanauza barakoa kwa Sh. 2,500 hadi 3,000.

“Wamekuwa wakitoa masharti kupitia mitandao ya kijamii kuwa hawauzi barakoa chini ya bei hiyo.”

“Sitawataja kwa leo, lakini nikiona tu wanauza kwa bei kubwa sitasita kuwachukulia hatua, maana mnakuja kuomba vibali, kumbe mnafanya mtaji,” alisema.

Alisisitiza kuwa barakoa zote ziuzwe kwa bei isiyozidi Sh. 1,500 badala ya bei ya sasa ilikuwa sokoni ya Sh. 2,500, ambayo Watanzania wengi inawapa changamoto ya kumudu.

Kwa upande mwingine, Bashungwa alivipongeza viwanda vya nguo vya A-Z na Sunflug kwa kuzalisha barakoa ambazo zinawasaidia Watanzania walio wengi, na amewaahidi serikali kuwapatia ushirikiano.

Aidha, alivitaka viwanda hivyo kuendelea kuzalisha kwa wingi ili wananchi wengi wa vijijini waweze kupata vifaa hivyo vya kujikinga na maambukizo ya ugonjwa wa corona.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliwataka wananchi wote wa mkoa huo kuchukua tahadhari zinazotolewa na Wizara ya Afya wanapotembelea maeneo yenye mikusanyiko.

Pia, alisisitiza kuwa ni vema sasa wafanyabiashara hao wakatengeneza barakoa kwa bei nafuu ili kuwezesha wananchi kuzinunua.

Akitoa taarifa kwa Waziri, Emmanuel Mgoma, mwakilishi wa kiwanda cha Sunflug, alisema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha barakoa 25,000 kwa siku.

Mwakilishi wa kiwanda cha A-Z, Slyvester Kazi, alisema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha barakoa 15,000 kwa siku.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live