Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa ameipongeza kampuni ya Huawei Tanzania kwa kukuza vipaji vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) akisema juhudi hizo zimesaidia na kuimarisha uwezo wa kuweza kuajiriwa na kupambana na ushindani wa kazi.
Waziri huyo ameeleza kuwa Tehama ni muhimu kwa maendeleo ya miundombinu ya Tanzania na Tehama ni mwezeshaji muhimu kufikia Dira ya Tanzania ya 2025 hasa katika mapinduzi ya viwanda.
Bashungwa ameyasema hayo wakati wa hafla ya utoaji Tuzo ya Mashindano ya Huawei Tanzania kuhusu Tehama 2019-2020 iliyofanyika Ijumaa Desemba 13, 2019 jijini Dar es Salaam.
Amesema Tehama inabeba jukumu la msingi katika kujenga uchumi wa Taifa, kutoa majibu kwa changamoto nyingi za kijamii, kuimarisha maendeleo jumuishi na endelevu kwa kukuza biashara, kutengeneza ajira na kuongeza tija na ufanisi.
Amebainisha kuwa kutokana na kasi ya maendeleo ya uchumi wa kidigitali ulimwenguni, ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia inabainisha kuwa mahitaji ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara kuhusu uhitaji wa ujuzi wa kidigitali ifikapo mwaka 2030 ni makubwa huku Tanzania ikiwa na uhaba wa wataalam wa fani hiyo.
“Katika kukuza ujuzi wa Tehama, vipaji ni mtaji muhimu. Kukosekana watu wenye ujuzi kutazuia uwezo wa kupokea, kumudu na kuendana na teknolojia mpya. Maendeleo ya Tehama yanahitaji kuwekwa wazi katika kuonyesha faida zake na kuwatambua wataalamu wa Tehama na kuwapa ujuzi wa kisasa pamoja na mafunzo ili kupata rasilimali watu wenye ushindani,” Amesema Bashungwa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Huawei Tanzania, Frank Zhou alibainisha kuwa Huawei inaona kuwa imepata fursa muhimu kufanya kazi na Serikali ya Tanzania na washirika wengine katika kuunganisha maeneo ya vijijini, kwa kujenga vituo vya gharama nafuu na vinavyotumia umeme wa jua.
“Huawei Tanzania inajivunia kuwa mstari wa mbele katika kujenga nguvu kazi ya kidigitali, kuwahudumia zaidi ya asilimia 35 ya Watanzania tangu tulipoanza shughuli zetu mwaka 2007, imetengeneza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 1,000 na kutoa mafunzo kwa wahandisi wa Tehama zaidi ya 2,000,’’ alisema Zhou.
Katika kukuza vipaji vya Tehama, Huawei Tanzania ina programu mbili zinazofanana; programu ya kwanza ni haki ya kazi ambayo ilifanyika Julai 2019 na ya pili ni mashindano ya Tehama, ambayo ni mchakato wa pili kwa mwaka wa utendaji wa Huawei Tanzania kushiriki hafla ya kidunia.
Zaidi ya wanafunzi 2,500 wa vyuo vikuu nchini, wanatarajia kushiriki shindano hilo litakalokuwa na mada mbalimbali, ikiwemo mitandao, utunzaji wa taarifa kwenye mtandao (cloud computing), nadharia na maendeleo ya mifumo ya komputa kufanya kazi za binadamu (artificial intelligence) na mkusanyiko mkubwa zaidi wa taarifa zinazoweza kuchambuliwa kwa komputa kuonyesha mifumo.