Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashe akoshwa mafanikio sekta ya kilimo

Nafaka Bashe Bashe akoshwa mafanikio sekta ya kilimo

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ajivunia mafanikio 10 yaliyopatikana mwaka 2023 katika sekta ya kilimo, huku akiweka wazi uamuzi wa Serikali kutaka kujitegemea katika uzalishaji, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo nchini.

Bashe ameyabainisha hayo kupitia taarifa aliyoitoa leo Januari Mosi, 2024 kwa vyombo vya habari kama salamu za mwaka mpya 2024 kwa wadau wa kilimo, huku akiyachambua mafanikio hayo katika sekta hiyo, ambayo ni mhimili wa maendeleo ya uchumi.

Ili kujitegemea kwa pembejeo, Waziri Bashe amebainisha kuwa serikali inaendelea na ujenzi miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini (ASA) na vituo ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari), ili kuyafikia mahitaji ya tani 652,250 za mbegu ifikapo mwaka 2030.

Mbali na pembejeo, pia waziri huyo amegusia kuongezeka kwa bajeti, jambo ambalo limeiwezesha wizara kutoa mchango unaostahili katika uchumi, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira, upatikanaji wa malighafi za viwanda na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa.

Wizara hiyo pia inaonekanaka kufurahia kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini kutoka tani 363,599 mwaka 2021/2022 hadi tani 580,628 mwaka 2022/2023, jambo lililochangiwa na Serikali kutoa mbolea ya ruzuku, na kuimarisha uwezo wa Kampuni ya Mbolea (TFC).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live