Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema serikali imeweka mifumo mizuri kuwezesha usalama wa chakula nchini na kwamba wawekezaji katika sekta ya kilimo hawaingiliwi katika kufanya maamuzi ya mauzo nje ya nchi.
Akizungumza katika mjadala wa Jopo la Mawaziri kuhusu Mwelekeo na Vipaumbele katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wakati wa Mkutano unaoendelea wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF 2023) jijini Dar es Salaam leo, Bashe ametaka wawekezaji kuondoa hofu kuhusu usalama nchini.
“Idadi kubwa ya wafanyabiashara na kampuni zinazowekeza nchini Tanzania zinafursa ya kuzalisha na kuuza katika nchi jirani zisizo unganishwa na bahari. Serikali inatambua kuwa kama tunahitaji kuongeza uzalishaji ni lazima tupunguze gharama za uzalishaji na hapa serikali imeweka mikakati ikiwa ni pamoja na kuweka ruzuku mfano kwenye mbolea,” amesema Waziri Bashe.