Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashe: Kama si mkulima usiwe kiongozi chama cha ushirika

82417 Bashe+pic Bashe: Kama si mkulima usiwe kiongozi chama cha ushirika

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Naibu Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe amepiga marufuku watu wasiokuwa wakulima kuongoza vyama vya ushirika kwa maelezo kuwa hawana msaada wowote zaidi ya kugeuka madalali.

Bashe ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 31, 2019 mjini Dodoma katika mkutano wa kitaifa wa wakulima wadogo nchini kwa ajili ya kutoa ilani ya wakulima kuhusu sekta ya kilimo.

Amesema viongozi ambao si wakulima wanawakandamiza wakulima badala ya kuwasaidia, kutumia fedha kwa maslahi binafsi.

"Nitumie jukwaa hili kuagiza viongozi wote wa vyama vya ushirika ambao si wakulima kutogombea nafasi hizo tena,  wawaache wakulima wenyewe ndio waongoze vyama hivyo. Haiwezekani wewe si mkulima halafu unaongoza wakulima huo ni udalali.”

"Serikali ina mpango wa kupitia mahesabu ya Amcos (vyama vya msingi vya ushirika) nchini kuona kama fedha za wakulima zipo salama au zimeliwa na kama tutakuta zimeliwa wahusika wote watachukuliwa hatua za kisheria," amesema Bashe.

Bashe ambaye ni mbunge wa Nzega Mjini amesema Serikali inatambua  mchango mkubwa unaotolewa na wakulima wadogo nchini kwa kuwa ndio wazalishaji wakubwa wa chakula ngazi ya familia. Mwenyekiti wa jukwaa la wakulima wadogo nchini, Janeth Nyamayahasi  amesema vyama vingi vya ushirika  nchini vinayumba kwa sababu viongozi wake si wakulima na hawajui thamani ya kilimo.

Chanzo: mwananchi.co.tz