Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ametaka wananchi wa Kata ya Sae waliovamia eneo la Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari-Uyole) kwa kujenga makazi, kufuata maelekezo ya Serikali na kuacha kuwasikiliza wanasiasa.
Bashe ametoa wito huo jana Jumanne, Agosti Mosi, 2023 wakati akitoa taarifa ya sekta ya kilimo wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya wakulima nanenane, ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini hapa, huku mgeni rasmi akiwa ni Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.
“Wananchi sikilizeni maelekezo ya Serikali msidanganyike na wanasiasa, mimi nilikuja na Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini Dk Tulia Ackson, nikatoa maelekezo lakini bado mnaendelea na ujenzi,” amesema Bashe.
Amesema kama Waziri mwenye dhamana hatoshindwa kubomoa makazi yao sambamba na kuwaomba wanasiasa kutowaunga mkono wananchi wanaovamia maeneo ya utafiti ili kulinda usalama wa chakula.
“Vituo vya utafiti ni usalama wa chakula, wanasiasa acheni kukaa migongoni mwa wananchi, sasa Serikali imeanza kuboresha miundombinu ya uzio kwenye vituo vyote vya utafiti wa mazao ya chakula na biashara ikiwepo Tari Mbeya,” amesema.
Aidha katika hatua nyingine Bashe amesema kuwa Serikali itaboresha kiwanja cha maonyesho ya nanenane Mkoa wa Mbeya ili kuweza kuendeleza maonyesho hata baada ya kuhitimishwa.
“Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kuboresha viwanja vya maonyesho ya nanenane kikiwepo cha Mbeya ili kuwa kitovu vya mafunzo ya kilimo, Uvuvi na mifugo,” amesema.
Amesema katika kuboresha sekta ya kilimo, Serikali imeongeza bajeti kutoka Sh200 bilioni mpaka Sh970 bilioni sawa na nyongeza ya asilimia 50 sambamba na kujenga miundombinu ya mabwawa 100 ya kilimo cha umwagiliaji.