Dar es Salaam. Serikali imesema baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ni chombo muhimu cha kuhimiza utendaji kazi hivyo ni vyema wajumbe wake wakawa waadilifu ili kutekeleza kwa ufanisi malengo ya wakala.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Aprili 5, 2019 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi) Joseph Nyamhanga katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge wakati wa uzinduzi wa baraza la kwanza la wafanyakazi wa Dart.
Amewataka wajumbe hao, kuwa wakweli na waadilifu katika kutoa maazimio yasiyo na upendeleo wala nia potofu kwa wakala na Serikali kwa ujumla.
Mtendaji Mkuu wa Dart, Ronald Lwakatare amesema baraza hilo ni chombo muhimu hasa katika suala la utawala bora na ni la kwanza tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo miaka 10 iliyopita.
"Limechelewa kuzinduliwa kwa sababu mipangilio haikuwa mizuri. Baraza hili litasaidia kutushauri hasa katika kipindi cha kuelekea bajeti, ambapo wataipitia bajeti ya Dart na kuiboresha,"amesema Lwakatare.
"Muwe chachu kwa wafanyakazi waliowatuma katika baraza hili. Natumai uanzishwaji wa baraza hi utasaidia kwa kiwango kikubwa kufanya maboresho mbalimbali sanjari na wakala kuleta tija," amesema Kunenge.