Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ziwa Tanganyika inavyojipanga kuacha kujiendesha kwa hasara

88855 Pic+bandari Bandari ziwa Tanganyika inavyojipanga kuacha kujiendesha kwa hasara

Tue, 17 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mamlaka ya bandari katika ziwa Tanganyika imesema inatarajia kupata faida na kuacha kujiendesha kwa hasara ifikapo Juni mwaka 2020.

Hayo yamebainishwa jana Jumatatu Desemba 16, 2019 na Meneja wa bandari za ziwa Tanganyika Percival Salama wakati akielezea utendaji wa bandari zilizopo katika ziwa hilo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2014/15 hadi 2018/19) bandari za ziwa hilo zimetengeneza hasara ya zaidi ya Sh13 bilioni, kwani matumizi yalikuwa Sh31 bilioni ikiwa miaka hiyo lakini mapato yalikuwa ni Sh18 bilioni.

"Mwaka 2014/15 mapato yalikuwa Sh2.09 bilioni, 2015/16 Sh2.66 bilioni, 2016/17 Sh4.14 bilioni, 2017/18 Sh5.69 bilioni, 2018/19 Sh4.148 lakini mwaka 2019/20 tumepanga kukusanya Sh7.6 bilioni ambayo faida itakuwa Sh400 milioni na mpaka sasa tunaendelea vizuri," alisema Salama.

Alisema katika mwaka huu wanatarajia kuongeza wingi wa mizigo wanayoihudumia hadi kufikia tani 210,000 kutoka tani 199,831 ambazo zilihudumiwa mwaka 2018/19 na tani 100,000 zilizohudumiwa mwaka 2014/2015.

 Aidha aliongeza hivi sasa Serikali imetoa Sh123.34 bilioni kwa ajili ya uboreshaji wa bandari katika ziwa hilo ambalo ni mpaka wa Tanzania na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.

Chanzo: mwananchi.co.tz