Bandari ya Tanga imefanikiwa kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 5 katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu, baada ya uwekezaji wa takribani shilingi Bilioni 429 uliofanywa na serikali katika bandari hiyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea Bandari ya Tanga ambapo amesema mapato hayo yametokana na kukamilika kwa gati mpya hatua ambayo imesaidia kuongezeka Kwa shehena ya meli za mizigo.
"Haya ndio mafanikio ya uwekezaji wa takribani Tsh. Bil 429 uliofanywa na Serikali katika Bandari ya Tanga ambao umesaidia kuongezeka Kwa shehena ya mizigo."
Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Peter Milanzi amesema ndani ya kipindi Cha miezi mitatu wamepokea Meli kubwa tano ambazo zimebeba zaidi ya shehena ya mizigo Tani 130,000; “Ajira za muda mfupi 100 zimeweza kupatikana kutoka na uingiaji wa Meli kubwa.”