Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ya Tanga mguu sawa soko la Kaskazini

C0154f89ba9029ede1ad795b30175db4 Bandari ya Tanga mguu sawa soko la Kaskazini

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: Habarileo

"Tunahitaji bandari hii ya Tanga sio sisi tu bali wafanyabiashara wote wakubwa na wadogo wenye bidhaa za kuingiza na kutoa kwa kutuma meli kwa upande huu wa Kaskazini wanahitaji bandari hii,” anasema Mkurugenzi wa kundi la kampuni la Neelkanth, Rashid Hamoud.

Anaongeza: “Ni bandari muhimu sana kwetu na kama meli ikiweza kutia nanga katika gati, wengi wetu tutaitumia na fursa za kupaa kwa Mkoa wa Tanga na mikoa jirani itakuwa kubwa sana."

Kampuni ya Neelkanth, Hamoud anasema inatumia Bandari ya Tanga kwa ajili ya kuingiza moja ya bidhaa zinazotumika kuzalisha chokaa inayojulikana kitaalamu kama petcoke.

Petcoke ni mapande ya mafuta ya petroli yanayozalishwa wakati wa mchakato wa kusafisha mafuta.

Kwa mujibu wa Hamoud, bidhaa nyingi hupatikana kutoka kwenye mafuta ghafi ikiwa ni pamoja na petroli, dizeli, mafuta ya ndege huku petcoke ikiwa ni mojawapo.

Bidhaa hii ndiyo inayotumika kuchoma mawe ya chokaa.

Anasema kwa mwaka wanaagiza zaidi ya tani laki moja na wakati wakiingiza katika bandari ya Tanga, hekaheka zake huwa si kidogo kutokana na meli kutia nanga bahari kuu, kiasi cha kilomita 1.7 na kisha kubebwa na matishari kuletwa bandarini.

"Hii ni gharama, ndio maana sisi kwa mzigo wa kiwanda cha Ndola, kilichopo Zambia tunaupitishia bandari ya Windhoek, Namibia," anasema.

Anasisitiza kuwa bandari itakapowezesha meli kubwa kutia nanga gatini petcoke inayoshushwa Namibia itashushwa Tanga kwa kuwa ni rahisi kuifikisha huko kutoka Tanga.

"Hii bandari ina fursa nyingi. Sisi tunauza bidhaa zetu Congo na hakika tulishakubaliana kwamba tunapopeleka mizigo yetu ya chokaa Congo basi malori hayo yarejee na shaba ambayo itapelekwa nje kupitia bandari ya Tanga," anasema Hamoud.

Anasema wafanyabiashara wa Congo wameshafika bandarini hapo kuangalia biashara hiyo lakini tatizo ni meli kushindwa kutia nanga gatini kutokana na ufupi wa kina.

Tatizo hilo la kina kifupi na la miaka mingi kwa Bandari ya Tanga, ambayo kiuhakika ni lango la Kaskazini, linatazamiwa kumalizika Machi wakati mradi wa awamu ya kwanza ya miradi miwili inayotekelezwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 468 kukamilika.

Miradi hiyo miwili ya uboreshaji wa bandari ya Tanga, mmoja umeshafikia asilimia 95 na kutarajiwa kuanza kufanyakazi Machi, mwingine upo katika asilimia 25 na utakamilika Oktoba.

Kukamilika kwa miradi hiyo miwili itawezesha meli kutia nanga katika gati na kupakua mizigo au kushusha abiria huku ikiwa haina shaka na kina cha bahari ambacho kwa sasa kimeondolewa kutoka mita tatu hadi 13.

"Kutokana na maboresho hayo sasa tutaweza kuhudumia mizigo ya zaidi ya tani milioni 2 kutoka kiwango cha sasa cha tani 730,000 kwa mwaka," anasema Mkuu wa idara ya utekelezaji, Colman Moshi wakati anazungumza na magazeti ya serikali hivi karibuni.

Bandari ya Tanga iliyo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ipo Kaskazini mwa Tanzania katika pwani ya Bahari ya Hindi na inatoa fursa kubwa ya kukua kwa uchumi wa watu binafsi na mkoa na hata taifa.

Miundombinu iliyopo kwenye bandai ya Tanga inaweza kuhudumia mikoa ya kaskazini na kwa nchi za jirani za Uganda, Sudani ya Kusini, DRC, Burundi na Rwanda kupitia bandari kavu ya Isaka na bandari ya Kigoma kwa kutumia miundombinu ya reli na barabara. Na pia inaweza kuhudumia Zambia na Malawi kupitia mipaka ya Kasumulu na Tunduma.

Bandari ya Tanga iliyoanzishwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1888 inajivunia kuwa na kingo za asili zinazozuia pepo za Kaskazini na kufanya ifanye kazi mwaka mzima.

Awali ilipoanza ilikuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa zaidi ya tani 1,200 na shughuli za upakuaji na upakiaji meli zimekuwa zikifanyika kwenye maji yenye kina kirefu na meli chache sana zenye uzito chini ya huo ziliweza kuhudumiwa bandarini (gatini).

Ilitengenezewa gati lenye urefu wa mita 381 na kufanyiwa kazi katika kina cha maji kuanzia mita 2 hadi 3.5 wakati wa bamvua dogo. Aidha, kwa asili gati lilijengwa na kina cha maji cha mita tano.

Kwa hiyo kuwapo kwa miradi hiyo miwili iliyoanza kwa nyakati tofauti na kuwa katika kiwango tofauti, wakati waandishi wa habari wanatembelea eneo, meli zilikuwa zimeshaanza kusogea kupakua na kupakia mizigo mita 200 kutoka gatini kutoka umbali wa awali wa kilomita 1.7 kwenye kina cha maji marefu maarufu kama nangani.

Kwa mujibu wa Moshi hatua iliyofikiwa na miradi hiyo inaonesha dhahiri kwamba kuanzia Machi gati itaanza kutumika rasmi kwa meli kubwa kwani kazi ya uchimbaji ili kuongeza kina kufikia mita 13 itakuwa imekamilika.

"Tumejiweka katika ushindani na bandari jirani. Kina kinaongezwa kuwezesha meli kufika bandarini na mitambo mipya na yenye uwezo mkubwa imeletwa kuongeza uwezo wa bandari. Kwa sasa kwa hali tuliyonayo tupo katika nafasi nzuri zaidi ya kutumia fursa ya ukaribu na wateja wetu kuongeza pato la taifa," alisema Moshi.

Moshi anasema bandari ya Tanga sasa ni shindani kutokana na ukweli kuwa ni jirani sana na mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi, Congo na Zambia.

Anasema kutokana na marekebisho ya tozo na kuimarishwa kwa usalama wa shehena, Bandari ya Tanga inabebwa na miundombinu ya barabara na reli iliyokamilika na inayoendelea kujengwa kuelekea maeneo ya kati ya Tanzania, Kaskazini na Kanda ya Ziwa.

Ushindani wa bandari hiyo pia unaelezwa na mwekezaji mwingine mkubwa wa Tanga wa kiwanda cha bidhaa za afya cha Tanga (TPPL).

Mkuu wa mipango na ugavi wa TPPL, Rajappan Ramesh anasema wanaitumia bandari ya Tanga kwa asilimia 80 lakini wanaamini gati ikianza kazi na meli kubwa kuingia gatini watatumia bandari hiyo kwa asilimia 100.

Anasema kwa sasa baadhi ya bidhaa zao zinashushwa bandari ya Mombasa na Dar es Salaam.

Ni dhahiri kwa mujibu wa mhandisi wa TPA, Fred Mahenge miradi hiyo miwili ya uboreshaji wa bandari ya Tanga yenye thamani ya Sh bilioni 468 umeiweka bandari ya Tanga katika uwezo mkubwa wa kushindana na bandari jirani nayo.

Anasema kwa kuongeza kina cha maji na ujenzi wa gati mbili zenye jumla ya urefu wa mita 450 na kuongezwa kwa vifaa, ambapo mitambo 11 imeshafika na mingine mitano ikiwa njiani kutaifanya bandari kuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena kwa muda mfupi na kwa ufanisi mkubwa.

Kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha meli za tani 50,000 na urefu wa mpaka mita 222 kutia nanga gatini. Gati linalojengwa lina uhai wa miaka 60.

Anasema kutokana na kuboreshwa kwa bandari malengo yao yamebadilika na kwamba mradi mzima ukikamilika Tanga inaweza kuhudumia shehena ya tani milioni tatu.

Ofisa mipango na takwimu wa Bandari ya Tanga, Joseph Mwambipile anasema mwaka huu wa fedha kwa maboresho yanayoendelea wamepanga kuhudumia meli zaidi ya 129 na hadi Desemba mwaka jana wamehudumia meli 88.

Anasema bandari hiyo yenye uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena za mizigo mbalimbali, mafuta na abiria imelenga kuhudumia makasha 20,000 na abiria 99,000 mara tu mradi kamili utakapokamilika Oktoba mwaka huu.

"Kwa kukamilika kwa miradi hii miwili Tanga tumejiweka katika ushindani kwani watu badala ya kupanga foleni watakuja Tanga kwa huduma ya haraka, nafuu na salama," anasema Colman Moshi.

Chanzo: Habarileo