Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ya Mtwara kusafirisha Korosho zote nchini

Mtwaraport Serikali yaridhia Bandari ya Mtwara kusafirisha Korosho zote nchini

Fri, 24 Sep 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, amesema Bandari ya Mtwara itatumika kusafirisha korosho na uamuzi huo hautabadilika, kwa kuwa ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Vilevile, amepiga marufuku matumizi ya kangomba kwenye mauzo ya zao hilo, akisisitiza utaratibu huo utachelewesha kuuzwa kwa bei nzuri na watu kuandaa mashamba kwa wakati.

Aliyasema hayo mjini Mtwara, juzi alipotembelea bandari hiyo, kwa lengo la kuangalia kama maelekezo ya Rais kuhusu korosho yote kusafirishwa kupitia bandari hiyo, yametekelezwa.

“Haya ni maelekezo ya serikali kwamba korosho yote huku, itapitia bandari hii, maagizo hayo ni ya Rais, hayatabadilika. Kwa hiyo, wote ambao wanataka kufanya biashara ya korosho wajipange.

“Zaidi ya hapo hapa bandarini wanafanya kazi saa 24, kwa hiyo meli ikija kama ni kupakia inapakia kwa muda na kasi sana, kwa sababu ya uwezo huo wa kufanya kazi muda wote," alisifu.

Waziri huyo alisema serikali imeshatoa kibali wanaosafirisha korosho kuleta Bandari ya Mtwara wanaruhusiwa kufanya hivyo kwa saa 24, hivyo wameshatengua kanuni zilizokuwa zinaelekeza baada ya saa 12, huwezi kusafirisha zao hilo.

Alisisitiza kuwa mtu akitaka kununua korosho, lazima apitishe kwenye bandari hiyo kwa kuwa gharama zimepunguzwa, hivyo kuokoa fedha nyingi, ambazo zingetumika kusafirisha kwa njia nyingine.

“Tunasisitiza si kwa sababu tunataka bandari hii ifanye kazi, bali uzoefu unaonyesha, kwamba korosho inaponunuliwa kutoka Mtwara, yenye ubora inaposafirishwa mpaka Dar es Salaam baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiiharibu kwa kuongeza vitu au kuweka isiyofaa," alisema.

Katika hatua nyingine, waziri huyo amepiga marufuku matumizi ya kangomba, kwa kuwa utaratibu huo utachelewesha kuuza kwa bei nzuri bidhaa hiyo na watu kuandaa mashamba kwa wakati.

Naibu Waziri wa kilimo, Hussein Bashe, alisema wataendelea kufanya kazi na Mamlaka ya Bandari na kupitia kikao kitakachofanyika Alhamisi, jijini Dar es Salaam, watajadili hoja mbalimbali zilizotolewa na wasafirishaji wa zao hilo.

Alizitaja baadhi ya hoja hizo ni gharama ya uhifadhi, upatikanaji wa makasha, muda wa kuhifadhi makasha ya wasafirishaji, ambao kwa sasa umeongezwa kutoka siku 14 mpaka 21, uwezo uliopo ni kuhifadhi makasha 13000 kwa wakati mmoja, hivyo hakuna tatizo.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Karim Mattaka, alisema wapo tayari kuhudumia shehena hiyo, kwa kuwa wameongeza uwezo wa kuhifadhi na kuhudumia korosho kwa kuongeza eneo na vifaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live