Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ya Mtwara inavyofungua fursa za uchumi Kusini

68e91d122a45a4cbabfd8240644ea6ec Bandari ya Mtwara inavyofungua fursa za uchumi Kusini

Tue, 23 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KUANZIA sasa wafanyabiashara nchini na nchi za jirani watakuwa wakinufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye Bandari ya Mtwara.

Bandari hiyo imeboreshwa kupitia ujenzi wa gati namba mbili uliogharimu Sh bilioni 157.8 na kuifanya iwe na uwezo sasa wa kuhudumia tani zinazofikia milioni moja na nusu za mizigo kwa mwaka.

Kabla ya hatua ya sasa iliyofanywa na serikali ya awamu ya tano kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), bandari hiyo wakati ina gati moja ilikuwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 tu kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba malengo ya mamlaka yake ni kujenga gati nne katika banadri hiyo ifikapo mwaka 2025 kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika mikoa ya kisini.

Bandari hiyo ambayo ni lango kuu la biashara na uchumi kwa mikoa ya kusini imejipanga kuwahudumia sio tu wateja wa ndani ya nchi, bali pia wateja wa nchi jirani zilizo kusini mwa Tanzania za Malawi, Zambia na Msumbiji.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Juma Kijavara, anasema kukamilika kwa mradi huo wa upanuzi wa bandari utarahisisha na kuimarisha uchumi hasa mikoa ya kusini mwa Tanzania kwa kuongeza pato la taifa, kutoa ajira na fursa mbalimbali za kiuwekezaji.

Kufadika kwa mikoa hiyo na bandari hiyo, pia kunatokana na uboreshaji wa barabara katika eneo hilo la kusini mwa Tanzania.

Kutokana na kuboreka kwa barabara na uwepo wa Ziwa Nyasa, sasa ni rahisi pia kwa wafanyabiashara wa Zambia na Malawi kutumia bandari ya Mtwara ambako ni karibu kulinganisha na bandari ya Dar es Salaam.

Mzigo unaweza kusafiri sasa kwa barabara kutoka Mtwara hadi Songea na kama mzigo ni wa Malawi au eneo la Msumbiji linalopakana na Ziwa Nyasa unaweza kusafiri kwa njia ya meli.

TPA ilijenga meli mbili za mizigo katika Ziwa Nyasa kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na nchi za SADC kuzitumia.

Lakini pia mzigo unaweza kusafiri kwa njia ya barabara kutokea Mtwara kupitia Songea na Njombe hadi Tunduma.

SHEHENA KUONGEZEKA MTWARA

Meneja huyo wa bandari, Kijavara anasema bandari hiyo tangu ijengwe mwaka 1953 wakati wa ukoloni, ilivunja rekodi kwa kusafirisha tani 377,590 za mizigo katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Anasema katika mwaka wa fedha 2018/19 bandari hiyo ilisafirisha tani 363,286 za shehena na mwaka 2014/15 ikasafirisha tani 296,577.

“Tofauti na gati zingine zilizopo nchini na nchi jirani, gati ya Bandari ya Mtwara ina kina cha asili cha mita 13 maji yanapokupwa. Hali hii inaifanya bandari hii kuwa bora zaidi katika ukanda wa kusini ikilinganishwa na kina cha mita 9.5 cha bandari za nchi jirani,” anasema Kijavara.

KOROSHO, SARUJI KUSAFIRISHWA MAJINI

Kwa mujibu wa Kijavara, shehena kubwa ya mizigo inayohudumiwa na bandari hiyo kwa sasa ni zao la korosho ambalo ndiyo zao kuu la biashara kwa mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Anataja shehana zingine kubwa zinazopitia kwenye bandari hiyo ni saruji inayozalishwa na kiwanda cha Dangote pamoja na mafuta.

KUPAKIA, KUSHUSHA MIZIGO

Kijavara anasema gati la sasa lililoboreshwa lenye urefu wa mita 300, linaweza kuhudumia meli zenye ukubwa wa tani 65,000 ikilinganishwa na gati la awali lililokuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa tani 45,000.

Kadhalika anasema eneo la kuhifadhia mizigo pia limepanuliwa na sasa lina ukubwa wa mita za mraba 79,000.

IMEKAMILIKA

Kijavara anasema kimsingi mkandarasi ameshakabidhi bandari hiyo kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania kutokana na kukamilika.

“Bandari imekamilika na kazi iliyobaki ni utendaji kazi kwani shilingi bilioni 157.8 zilizowekwa na Serikali, matokeo yake yanatakiwa kuonekana na ni kwa kuongeza kipato tu lakini pia ufanisi,” anasema Kijavara.

KUKOMESHA ‘WIZI’ WA MAFUTA

Meneja huyo anasema ile hali ya kukadiria mafuta yanayoingia kupitia kwenye bandari hiyo ya Mtwara imefikia ukingoni baada ya ujenzi wa bomba la kupima mafuta (flow meter).

Wakati HabariLEO likiwa katika bandari hiyo hivi karibuni, ujenzi wa nyenzo hiyo ya kupimia mafuta ulikuwa umefikia asilimia 98.

Kijavara anasema kipimo hicho ni kwa ajili ya mafuta ya dizeli na petrol yatakayopitishwa ktika bandari hiyo, hatua itakayoiongezea Serikali kipato kwa kuwa hakuna njia ya kuiba au kukadiria chini ya kiwango mafuta yanayoingia nchini.

Meneja hiyo anasema kuwa hapo awali, uhakiki wa mafuta yaliyopitia bandarini hapo na tozo mbalimbali zilikuwa zikikadiriwa kwa macho zaidi lakini sasa uwepo wa bomba la kupimia mafuta utabadilisha hali hiyo na matumaini ni kuongeza kipato cha Serikali.

“Sasa tutapima mafuta kupitia flow meter ili tozo za Serikali zikusanywe zote na mfanyabiashara alipe tozo stahiki. Lengo letu ni kuona tunapokea meli za mafuta nyingi ili biashara hiyo ianze kutunufaisha hususani kwa wafanyabiashara wa upande wa nchi ya Malawi na kwingineko,” anasema meneja huyo.

Kukamilika kwa ‘flow meter’ hiyo kutaongeza idadi ya bandari zenye kifaa hicho adhimu kutoka mbili hadi tatu. Bandari nyingine zenye flow meter ni za Dar es Salaam na Tanga.

TASAC YAPONGEZA

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Wakala wa Meli nchini (TASAC), Mussa Mandia, anasema kuwa hatua iliyofikiwa na TPA ni nzuri na kwamba ‘flow meter’ itapunguza sintofahamu iliyokuwapo hapo awali na badala yake kuwa mtaji wa kunyanyua uchumi wa nchi.

“Ufungaji wa vifaa hivi itaongeza ufanisi kwa kupunguza muda wa meli kukaa bandarini. Pia utaongeza usalama wa mizigo inayoshushwa bandarini ikiwemo kupunguza au kumaliza wizi wa mafuta,” anasema Mandia.

Mjumbe mwingine wa bodi hiyo, Renatus Mkinga anasema: “Zamani kidogo wafanyabiashara walipinga sana uwekaji wa ‘flow meter’ kwa sababu walikuwa ‘wakiipiga’ Serikali lakini Rais John Magufuli alilisimamia na kuhakikisha kuwa wizi huu unakomeshwa na Serikali inapata kipato chake halali.”

Chanzo: habarileo.co.tz