Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ya Mkwaja yaingiza mamilioni ya ‘mkwanja’

6b12d3f5fb6d57038e39fab3eee281c0 Bandari ya Mkwaja yaingiza mamilioni ya ‘mkwanja’

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Bandari ya Mkwaja iliyopo wilayani Pangani mkoani Tanga iliyorasimishwa mwaka mmoja uliopita na kuwa chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), kuanzia Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu imeingiza pato la Sh 48,538,943.

Ofisa msimamizi wa bandari hiyo, Boniphace Mwangulube alisema pato hilo linatokana na huduma walizotoa katika shehena mchanganyiko walizohudumia.

Kwa mujibu wa msimamizi huyo, bandari hiyo imekuwa ikitumika kwa ajili ya mizigo mchanganyiko ikiwamo mifugo kama ng’ombe, kondoo na mbuzi.

Ofisa huyo wa TPA alisema kuanzia Julai hadi Januari mwaka huu wamesafirisha ng’ombe 12,956 na mbuzi 3,022.

Alisema wakati wavuvi wanatumia bandari hiyo kutengeneza dagaa kwa ajili ya kuwasafirisha kwenye mikoa ya jirani hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Rwanda; mifugo, mkaa na mbao ni bidhaa ambazo zimekuwa pia zikipitia bandari hiyo kwenda Zanzibar.

Ingawa wavuvi hawatozwi kwa bidhaa zao wanazoingiza, walisema kuwepo kwa urasimishaji uliofanyika mwaka mmoja sasa umewasaidia kuwahakikishia usalama wa mali zao.

Ali Chande alisema wamekuwa katika mazingira mazuri zaidi ya kibiashara kutokana na kurasimishwa kwa bandari ila wanachoomba TPA wafanye hima kuwasaidia kupata ghala la kuhifadhia bidhaa.

Alisema sehemu hiyo ambayo ipo wazi wakati mwingine inakumbwa na upepo mkali, hivyo katika urasimishaji huo serikali ingepeleka miradi kuimarisha zaidi bandari hiyo ambayo hupokea majahazi hadi 15.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa bandari hiyo, Bwasha Mswahili alisema kuna mabadiliko ambayo wanatarajia yatokee hasa ya kuwa na utaratibu wa upatikanaji wa huduma.

Alisema kijiji hicho ambacho bandari ipo kina shughuli nyingi za kilimo na uvuvi kwa hiyo uwepo wa bandari unaondoa mahangaiko ya awali ya mizigo kupata misukosuko kutoka kwa mamlaka.

Bandari ya Mkwaja ni miongoni mwa bandari kadhaa bubu ambazo zimerasimishwa na kuingizwa katika utaratibu wa kiusalama na kimapato wenye usimamizi wa serikali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz