Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari ya Dar es Salaam kutangazwa kimataifa.

Logotpa.png Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na wadau wa bandari inaandaa mkakati wa kuitangaza Bandari ya Dar es Salaam kimataifa ili kuongeza kiwango cha mizigo ya nje kupitia bandari hiyo.

Pia mkakati huo utahusu kuzitangaza kimataifa Bandari za Tanga na Mtwara. Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Erick Hamisi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na HabariLEO.

Alisema Bandari ya Dar es Salaam haijatangazwa vya kutosha, hivyo wamekubaliana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kuandaa kikao kitakachowashirikisha wadau wengine wa bandari ili kuja na mkakati wa kuitangaza kwa pamoja kimataifa.

Pia alisema mkakati huo pia utazihusisha Balozi za Tanzania nje ya nchi kwa kuziandalia taarifa sahihi kuhusu upanuzi wa bandari unaofanyika, uwezo wake na taarifa nyingine muhimu ambazo watazitumia katika kuzitangaza bandari hizo.

“Nimepanga niongee nao kwa njia ya ‘zoom’ mabalozi wote wanaotuzunguka kwanza, nimeshaanza utaratibu wa kupata kibali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, taratibu zikikamilika nitaongea nao kuwaambia maeneo ambayo tutaomba watusaidie kuzitangaza bandari zetu,” alisema Hamisi.

Alisema mpaka sasa mabalozi wengi wanafanya kazi nzuri ya kuzitangaza bandari za Tanzania na ndiyo maana soko la Rwanda na Burundi wamelikamata kwa asilimia kubwa.

Juzi, Hamisi alikutana na Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula kwa lengo la kujadili namna gani TPA na sekta binafsi wanaweza kushirikiana katika kuzitangaza Bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga katika ngazi ya kimataifa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz