Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka Uongozi wa Shirika la Bandari la Zanzibar kuongeza kasi ya kiutendaji ili kurahisisha Huduma zao kwa wale wanaowahudumia.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipofanya ziara ya kukagua eneo linalotumika kushushia na kupakia Makontena Bandarini Malindi Jijini Zanzibar.
Amesema Muamko wa Wafanyabiashara kwa Wenye Meli za Mizigo ni mkubwa ambao umeamsha ari kutokana na Uongozi wa Awamu ya Nane ili wananchi wapate huduma mbali mbali kwa urahisi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema muitiko wa Meli kubwa za Kimataifa kuja kushusha Mizigo Zanzibar ni jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi kuwaomba na kuwashawishi Wafanyabiashara kuweza kuleta mizigo yao Zanzibar kwa kuwepo kwa taratibu nzuri zinazowaongoza katika Shughuli zao.
Hemed amesema ni vyema kwa Uongozi wa Shirika hilo kuwa na urafiki na Wafanyabiashara kwa kuwapa muongozo mzuri wa kusimamia ushushwaji wa mizigo ili kuepuka Meli hizo kuchukua muda mrefu jambo ambalo linapelekea kuchelewesha kufunga gati Meli nyengine zinazofika Zanzibar na kupelekea meli kulipa gharama kubwa hatua ambayo inakwenda kuwagharimu wananchi kwa kuuziwa bidhaa kwa gharama ya juu.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza wafanyabiashara wanaotakiwa kutoa mizigo yao ambao muda wao umemaliza kufanya haraka kutoa mizigo yao ili kupisha meli nyengine ziweze kushusha mizigo na wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amekemea tabia ya Wafanyabiashara wanaotoa mizigo wakati wa usiku ambao hufanya hivyo kwa kutaka kufanya udanganyifu kwa lengo la kuikosesha Serikali mapato, na kueleza kuwa hatua hiyo inapelekea kuwepo kwa mwanya wa vitendo vya rushwa eneo hilo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameonesha kufurahishwa kwake kwa Shirika la Bandari Zanzibar kuandaa mpango wa kuanzisha Kituo cha (One Stop Center) ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zote za uingizaji na utowaji wa makontena Bandarini hapo.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar Akif Ali Khamis ameeleza kuwa licha ya udogo wa eneo la kuhifadhia Makontena bado wanaendelea kuzungumza na wafanyabiashara wanaoleta mizigo kutoa mizigo kwa wakati hatua ambayo inatoa nafasi kwa wafanyabiashara wengine kushusha mizigo yao na kutanua uchumi wa Nchi jambo ambalo ndio ndoto ya Serikali ya Awamu ya Nane.
Aidha Ndugu Akif amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa kuna muamko mkubwa kwa wafanyabiashara kushusha mizigo Zanzibar ambapo kwa mwaka jana Jumla ya makontena 3200 yalishushwa na mwaka huu wameshusha jumla ya 4600 hatua ambayo inasaidia kuongezeka kwa mapato ya nchi.