Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari Mtwara tayari kutekeleza agizo la Samia

Da1e8494bbf073f8fea0ef94e02a08a3.jpeg Bandari Mtwara tayari kutekeleza agizo la Samia

Sat, 12 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imeanza kufanyia kazi maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mzigo wote wa korosho zinazozalishwa katika mikoa ya kusini unapitia katika bandari ya Mtwara.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Marco Gaguti alisema bandari hiyo iko tayari kupokea mzigo huo na mingine mingi kwani imepanuliwa na ina vifaa

vyote muhimu.

“Kama ambavyo maelekezo yametolewa na Rais, kuanzia mwaka huu korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Ukanda wa Kusini zitapitia katika Bandari ya Mtwara ambayo iko tayari,” alisisitiza.

Alisema mwaka huu kwa mkoa wa Mtwara pekee matarajio ni kuzalisha tani 170,000 za korosho kupitia bandari hiyo na kwamba wanafanya pia utaratibu wa kuona kiwanda cha saruji cha Dangote kinatumia bandari ya Mtwara kwa asilimia 100.

Alifafanua kwamba mbali

na kuongeza gati jipya, bandari hiyo pia imeongeza eneo la kushughulikia korosho na mizigo mingine kutoka mita za upana 30,000 mpaka 50,000.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma zipitie katika Bandari ya Mtwara.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi, alisema wanaangalia namna ya kupunguza tozo kuvutia wafanyabiashara wengi kutumia bandari ya Mtwara.

“Kwa kuwa sasa tunataka kuvutia wafanyabiashara wengi kutumia bandari ya Mtwara, tozo za hapa haziwezi kuwa sawa na za bandari ya Dar es Salaam,” alisema.

Hamissi aliyewasili Mtwara tangu Jumatatu akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Mipango na Uwekezaji wa Bodi ya TPA, alisema wameunda timu maalumu ya kuzungumza na uongozi wa Dangote ili watumie bandari hiyo kwa asilimia 100 katika maeneo yote yenye bandari Tanzania.

Kampuni ya Dangote imekuwa ikisafirisha saruji

katika mikoa yenye bandari kama Dar es Salaam kwa njia ya barabara, hali inayochangia uharibifu wa barabara.

Gazeti hili limeshuhudia maeneo kadhaa ya barabara ya Lindi - Mtwara kama vile Kiranjeranje na Mandawa yakifanyiwa ukarabati mkubwa.

Imebainika hatua ya wafanyabiashara kupitishia korosho katika bandari ya Dar es Salaam ilianza serikali iliporuhusu kila mwenye korosho yake kuisafirisha kupitia kokote.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Juma Kijavara, aliliambia HabariLEO kwamba

baada ya wafanyabiashara kunogewa na kupitishia korosho zao Dar es Salaam walikuwa wameanza kuitelekeza bandari ya Mtwara. Alisema kinachowavutia ni urahisi wa gharama za mabehewa ikilinganishwa na bandari ya Mtwara.

Alisema hatua wanazochukua sasa mbali ya kupunguza tozo ni pamoja na kuangalia muda wa behewa kukaa bandarini bila kuanza kulipiwa, jambo ambalo pia linapandisha gharama za behewa.

Imeandikwa Hamisi Kibari na Sijawa Omari.

Chanzo: www.habarileo.co.tz