Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari Mtwara na mageuzi yanayogusa nyoyo za wateja

Bandari Mtwaratt Bandari Mtwara na mageuzi yanayogusa nyoyo za wateja

Tue, 15 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Huduma bora, mitambo na vifaa vya kisasa, usalama wa mizigo, yadi kubwa ya kuhifadhia mizigo, ujenzi wa gati jipya, kufungwa kwa ‘flow meter’, utendaji makini wa watumishi wa bandari, umeifanya Bandari ya Mtwara kuwa kimbilio la wafanyabiashara na kuufungua uchumi wa mikoa ya kusini na nchi jirani kwa kasi.

Serikali iliamua kufanya upanuzi wa bandari hii kwa kujenga gati jipya lenye urefu wa kina cha mita 13.5 na urefu wa mita 300 na kuifanya kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa zenye uzito wa hadi tani 65,000 kwa muda mfupi.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdillahi Urio, anasema Bandari ya Mtwara ni moja ya bandari kuu tatu ikiwemo bandari za Dar es Salaam na Tanga.

Anasema Bandari ya Mtwara imejengwa mwaka 1950 ikiwa na gati lenye urefu wa mita 385 na kina cha mita 9.5 huku uwezo wake wa kuhudumia shehena ya mizigo ilikuwa tani 400,000 tu kwa mwaka, lakini ujenzi wa gati jipya umeifanya bandari hii kuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni moja ya mizigo kwa mwaka.

Urio anabainisha kuwa Bandari ya Mtwara inahudumia shehena ya mizigo zikiwemo bidhaa za kilimo kama vile korosho, bidhaa za viwandani ikiwemo saruji, makaa ya mawe, mafuta, bidhaa za miradi na pia ina uwezo wa kuhudumia shehena za magari.

Anasema haya yote yanawezekana kutokana na uwekezaji mkubwa wa Sh bilioni 157 ambao serikali imeufanya kwa kujenga gati jipya na la kisasa lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa, pia uwekezaji katika kununua vifaa vya kisasa vya kupakia na kupakua mizigo kwenye meli.

Amevitaja vifaa hivyo kuwa ni winchi inayotembea yenye uwezo wa kubeba tani 100, winchi tatu zinazotembea zenye uwezo wa kubeba tani 30 hadi 50, trekta 14 na trela 20 za kubeba kontena, Forklift 15 za kubeba tani tatu hadi 42, Reach Stacker tatu za kubeba tani 45, Empty Handler tano za kubeba tani nane hadi 12, Spreaders 10 na vifaa vingine vingi.

“Bandari ya Mtwara ina vivutio mbalimbali ili wateja waendelee kuitumia bandari hii. Kwanza ufanisi katika utendaji kazi ni mkubwa, tunatoa huduma saa 24 kila siku, tunatumia mifumo ya kielektroniki ikiwemo Harbour View System, Cargo System, Payment na Billing System kwa ajili ya kuhudumia meli na mizigo,”anasema Urio.

Anaongeza “Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa uboreshaji mkubwa wa miundombinu na vifaa katika Bandari ya Mtwara, pia tunaishukuru Serikali ya Mkoa wa Mtwara kwa kufanya kazi kwa karibu na bandari hii, tunatoa wito kwa wafanyabiashara wapitishe mizigo yao kutoka nje ya nchi au kwenda nje ya nchi kwenye bandari hii.”

Eneo la Uwekezaji Urio anasema Bandari ya Mtwara ina eneo la hekta 2,600 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali, hivyo anatoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya viwanda waitumie fursa hii kwa kuwa eneo lipo karibu kabisa na bandari.

Wadau wa Bandari Wafanyabiashara wanaoutumia Bandari ya Mtwara, wameeleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa na bandari hii.

Miongoni mwa wafanyabiashara hao ni Kampuni ya Mafuta ya Oilcom Tanzania Ltd, Tawi la Mtwara, Kampuni ya Meli ya Alghubra Marine Services ya Zanzibar, Kampuni ya Uwakala wa Meli ya Southern Shipping Services Ltd na Kampuni ya Makaa ya Mawe ya Ruvuma Coal Ltd Tawi la Mtwara.

Mwakilishi wa Kampuni ya Makaa ya Mawe ya Ruvuma Coal Ltd, Saidi Gadafi, anabainisha kuwa kabla ya maboresho ya Bandari ya Mtwara, walikuwa wakisafirisha tani 30,000 za makaa ya mawe kwenda China na India kila baada ya miezi mitatu, lakini kwa sasa wanasafirisha tani 55,000 kila baada ya mwezi mmoja na nusu.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inatuunga mkono na tunatarajia kufungua soko jipya Mashariki ya Kati. Tunatoa wito kwa wafanyabiashara wengine waje kuitumia Bandari ya Mtwara kwa kuwa ina huduma bora, hakuna ucheleweshaji, ushirikiano na menejimenti ni mzuri,”anasema Gadafi.

Ofisa Utekelezaji wa Kampuni ya Uwakala wa Meli ya Southern Shipping Services Ltd, Esthersia Mallya, anasema kuwa tangu kujengwa kwa gati jipya, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika Bandari ya Mtwara. Mallya anaeleza kuwa hivi karibuni wamepokea meli ya tani 5,000 inayochukua saruji kutoka Mtwara kwenda Comoro na waliipakia kwa siku moja tu tofauti na zamani walikuwa wakiipakia kwa siku saba hadi kumi.

“Kuna maboresho makubwa kwenye bandari vikiwemo vifaa vya kisasa, nguvu kazi ya kutosha, ankara zinapatikana kwa wakati, tunashughulika na usafirishaji wa saruji kwa meli zinazoenda Zanzibar, Comoro na Msumbiji, hakuna ucheleweshaji wa meli, tunaipongeza Serikali ya Rais Samia kwa maboresho haya,”anasema Mallya.

Mwakilishi wa Kampuni ya Mafuta ya Oilcom Tanzania Ltd, Jackson Tumwanga, anasema kuwa Oilcom ni wadau wakubwa wa Bandari ya Mtwara katika uingizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi kwa mikoa ya kusini mwa Tanzania.

Tumwanga anasema kabla ya kupanuliwa kwa Bandari ya Mtwara, meli zao zilikuwa zikitumia Bandari ya Dar es Salaam ambapo mafuta yalipakuliwa na kupakiwa tena kwenye meli ndogo na kuletwa Mtwara hali iliyowafanya watumie gharama kubwa, lakini kwa sasa meli zao za mafuta zinakwenda moja kwa moja katika Bandari ya Mtwara baada ya kuboreshwa.

“Hivi sasa tunaleta mzigo wa mafuta kutoka nje ya nchi moja kwa moja mpaka hapa Bandari ya Mtwara. Tunaridhika na huduma za bandari, vipimo vya ubora wa mafuta, kwa hiyo wafanyabiashara wenzetu waje kutumia Bandari ya Mtwara kwa sababu hakuna foleni ya meli na nafasi ipo ya kutosha,”anasema Tumwanga.

Anaongeza, “Kila mwezi Oilcom tunapokea meli ya mafuta katika bandari hii, tunaingiza lita milioni 4.8 za petroli na lita milioni 4.8 za dizeli, tupo kwenye mchakato wa kujenga matangi mawili ambapo tangi moja litakuwa la lita milioni 12.5, kwa hiyo tutakuwa na matangi ya lita milioni 25 za mafuta ambayo pia tutayauza katika nchi jirani, tunaishukuru serikali kwa tuwekea ‘flow meter’ hapa inatusaidia kujua kiasi halisi cha mafuta tunachoingiza.”

Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli ya Alghubra Marine Services, Abdulsamad Mohamed Suleiman, anasema kampuni yao inasafirisha saruji kutoka Mtwara kwenda Pemba, Unguja na Comoro. Suleiman anasema kabla ya upanuzi, mazingira ya kazi yalikuwa magumu lakini baada ya maboresho, Bandari ya Mtwara imekuwa miongoni mwa bandari bora hapa nchini kwa kutoa huduma za uhakika na kwa muda mfupi.

“Bandari ya Mtwara kwa sasa hakuna foleni, kuna mashine za kisasa na za kutosha za kushusha na kupakia mizigo, meli yetu ina uwezo wa kubeba tani 880 za saruji na tumekodi meli nyingine yenye uwezo kama huu, huduma ya bandari ni nzuri sana,”anasema Suleiman.

Chanzo: www.habarileo.co.tz