Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari Dar yataja sababu ongezeko mizigo

7d0c2ad94c30c9dcc0e6f1e7f2a10d7b.jpeg Bandari Dar yataja sababu ongezeko mizigo

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KIWANGO cha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kimeongezeka katika miaka mitano iliyopita kutoka tani milioni 13.8 mwaka 2015/2016 hadi tani milioni 16.1 mwaka 2019/2020.

Miongoni mwa nchi ambazo mizigo yake imepitishwa kwenye bandari hiyo katika miaka mitano iliyopita ni Tanzania yenyewe, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema, aliyasema hayo alipozungumza na HabariLEO ofisini kwake.

Lema alisema katika mwaka 2016/2017, bandari hiyo ilihudumia jumla ya tani milioni 13.3 za mizigo, lakini pia mwaka 2017/2018 ilihudumia tani milioni 14.9 na mwaka 2018/2019, tani milioni 15.7 za mizigo ya nchi hizo.

Kuongezeka kwa kiwango hicho cha mizigo kunatokana na sababu mbalimbali yakiwemo maboresho ya bandari kwa kuongeza kina cha magati kutoka mita 8.5 hadi kufikia mita 14.5.

Lema alisema kuongezwa kwa kina cha Gati Namba Moja hadi Gati Namba Saba, kumeziwezesha meli kubwa kutia nanga katika bandari hiyo.

"Baada ya maboresha haya ya kuongeza kina cha gati zetu hadi kufikia mita 14.5, faida ambazo tumeanza kuzipata ni pamoja na meli zenye ujazo mkubwa kuanzia tani 40,000 hadi tani 50,000 kutia nanga kwenye gati hizi ikilinganishwa na zamani ambapo zilikuwa zinakuja meli ndogo zenye ujazo wa tani 15,000 au tani 30,000, na meli kubwa zinazokuja zina urefu wa mita zaidi ya 200," alisema Lema.

Nafasi ya kijiografia ya Tanzania imetajwa kuwa sababu nyingine iliyochangia kuongeza mizigo kwenye bandari hiyo.

Lema alisema nchi nane zisizo na bahari ambazo zimepakana na Tanzania zinatumia Bandari ya Dar es Salaam zikiongozwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kupitisha kiasi kikubwa cha mizigo kinachofikia tani milioni 1.9 mwaka 2019/2020.

Lingine lililofanikisha ufanisi huo ni udhibiti wa vitendo vya wizi na uhalifu kwa kuimarisha ulinzi na usalama.

Lema alisema hatua hiyo imechangia kuongezeka kwa kiwango cha mizigo inayohudumiwa na bandari hiyo.

"Bandari ya Dar es Salaam iko salama na wateja wanapata mizigo yao kama walivyoagiza, ufanisi katika utendaji umeimarika na kuwafanya wateja kupata mizigo yoa mapema zaidi, kwa hiyo tunawapa uhakika wa kuendelea kuwahudumia vizuri wateja wetu wa ndani na nje ya nchi," alisema.

Kukamilika na kuanza kutumika kwa gati jipya la magari na yadi ya kuhifadhi magari hayo, kumeongeza kiwango cha magari yanayoshushwa kwenye bandari hiyo.

Lema alisema gati jipya linalojulikana kama Gati 0 lenye urefu wa mita 320 limeongeza ufanisi katika ushushaji wa magari zaidi ya 100 kwa saa ikilinganishwa na magari 50 hadi 70 ya awali.

"Muda unaotumika kupakua meli yenye magari na kuondoka ni siku moja na ikizidi sana ni siku moja na nusu ikilinganishwa na siku tatu zilizokuwa zikitumika hapo kabla, kwa mfano meli yenye magari 1,100 inachukua siku moja na nusu tu kumaliza kushusha," alisema.

Lema alisema gharama wanazotozwa wateja katika Bandari ya Dar es Salaam ni ndogo ili wapate faida na serikali nayo ipate mapato kwa maendeleo ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz