Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari Dar yaita mwekezaji mpya

Mahakama Kuamua Mustakabali Wa Mkataba Wa Bandari Leo Bandari Dar yaita mwekezaji mpya

Tue, 20 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema pamoja na maboresho yaliyofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam, kuna haja ya kuongezwa gati namba 13 hadi 15 ili kuongeza ufanisi wa bandari hiyo.

Katika kufanikisha kazi hiyo, Profesa Mbarawa amezikaribisha kampuni za uwekezaji kutoka Misri kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji kwenye ujenzi wa magati hayo.

Kauli ya Profesa Mbarawa inatokana na kile alichoeleza licha ya maboresho yaliyofanywa na Serikali katika bandari hiyo, bado kuna msongamano wa meli, akidokeza kwa sasa zipo takriban 18 zinasubiri kuhudumiwa.

Hata hivyo, Oktoba 22, mwaka jana Serikali ilisaini mkataba na Kampuni ya Dubai Port World (DP World) wa ukodishaji na uendeshaji wa gati namba 4 hadi 7 wa Bandari ya Dar es Salaam.

Kulingana na mkataba huo, gati namba 0 hadi 3 katika bandari hiyo yatatumiwa kwa pamoja kati ya DP World na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa ajili ya shughuli nyingine za kibiashara na Serikali.

Hatua hiyo ilifanyika ikilenga kile kilichoelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kuwa ni kuongeza ufanisi wa utendaji katika Bandari ya Dar es Salaam.

Profesa Mbarawa amesema hayo leo Jumatatu Februari 18, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao cha Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania na Wizara ya Uchukuzi ya Misri kilichohusu ushirikiano wa uwekezaji katika sekta ya uchukuzi.

Amesema kuna haja ya kuongeza magati katika bandari hiyo, ili kupunguza msongamano wa meli zinazohudumiwa.

Amesema magati hayo anatarajia yajengwe kwa ushirikiano na wawekezaji kutoka katika taifa la Misri. Kuhusu ushirikiano kati ya Misri na Tanzania, alisema utawezesha watu wa mataifa hayo kubadilishana ujuzi na hatimaye kukuza uchumi.

Akihitimisha kikao hicho, Profesa Mbarawa amemuomba Waziri wa Uchukuzi wa Misri kuridhia kuwapokea Watanzania watakaokwenda kujifunza uendeshaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Ombi hilo lilitokana na kile alichoeleza, Misri ina uzoefu mkubwa wa uendeshaji wa SGR, hivyo ni vema wakati Tanzania Julai mwaka huu ikitarajia kuanza mradi huo wawepo wataalamu waliopata ujuzi huo.

Ombi lingine ni ushirikiano kati ya Chuo cha Baharia cha Tanzania na Taasisi ya Mafunzo ya Ubaharia ya Misri. Naye Waziri wa Uchukuzi wa Misri, Luteni Jenerali Kamel Alwazeer ameelezea kuridhishwa na fursa za uwekezaji katika sekta ya uchukuzi nchini huku akisema nchi yake ipo tayari kuwekeza Tanzania.

“Tutawasilisha maswali yetu kupitia ubalozi wetu wa hapa (Tanzania) kwenda Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania, ili tupate ufafanuzi kwa ajili ya kuanza uwekezaji," amesema Alwazeer.

Hata hivyo, amesema hatua ya mwendelezo wa kikao hicho, amemkaribisha Profesa Mbarawa kwenda Misri kwa mazungumzo kama hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live