Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari Dar, ATCL kuvuna neema DRC kujiunga EAC

D818cc3cd43720fe7e2f313c8de25250 Bandari Dar, ATCL kuvuna neema DRC kujiunga EAC

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bandari ya Dar es Salaam na Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) wamesema ujio wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika Jumuiya ya Afrika Mashaariki (EAC) utaongeza kiwango na fursa ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Juma Kijavara, alilieleza HabariLEO kuwa kwa sasa mzigo mkubwa unaohudumiwa na bandari hiyo ni wa Rwanda na Zambia lakini kwa DRC mzigo bado mdogo.

Kijavara alisema uamuzi wa wakuu wa nchi EAC kukubali DRC ijiunge kwenye jumuiya hiyo utasaidia kuboresha biashara kati ya nchi hiyo na Tanzania kwa kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni kiungo katika usafirishaji wa bidhaa kwenda kwenye nchi za maziwa makuu na nchi nyingine jirani.

“DRC kujiunga EAC itatusaidia kuongeza mzigo ambao unahudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwenda DRC. Mzigo wa DRC baada ya kushushwa Bandari ya Dar es Salaam, unaweza kukaa kwa siku 30 bila malipo,”alisema Kijavara.

Aliongeza”Mwaka 2020/21, tumehudumia tani milioni 1.9 kwa ajili ya nchi ya DRC, na Julai 2021 hadi Februari mwaka huu tumehudumia tani milioni 1.8 ambazo ni juu ya lengo la kuhudumia tani milioni 1.4 kwa kipindi hicho.”

Akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Azam hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Erick Hamisi alisema Bandari ya Dar es Salaam inahudumia asilimia 35 ya mizigo inayokwenda DRC na sasa wanajipanga kiasi hicho kiongozeke hadi kufikia asilimia 50.

Hamisi alisema kwa kuanzia kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa,TPA inajipanga kuhudumia tani milioni tatu za mizigo kwenda DRC.

“Mpango wetu ni kufika sehemu ambako kuna mzigo mkubwa; tukienda Lubumbashi, Katanga Province, soko hili ni muhimu kwa Bandari ya Dar es Salaam,”alisema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ATCL, Josephat Kagirwa alisema ujio wa DRC katika EAC utaongeza idadi ya wasafiri na wafanyabiashara wanaotumia ndege za kampuni hiyo kwenda nchini humo.

Kagirwa alisema kuingia kwa DRC kutafanya mambo mengi ya kibiashara kufunguka ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya mizigo, abiria na wafanyabiashara wanaoutumia ndege za ATCL ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

“Vikwazo vingi vitapunguzwa kwa sababu tayari DRC wanakuwa wanachama, kwetu itakuwa rahisi kufanya safari za huko na kuongeza abiria na mizigo, tumelipokea kwa furaha kwa sababu soko letu litakuwa kubwa,” alisema Kagirwa.

Alisema biashara ya ATCL nchini DRC ni nzuri kwa sababu kwa safari wanazofanya kwenda Lubumbashi kumekuwa na abiria wengi na ndege inajaa kwa asilimia 75 mpaka 80, pia uhitaji ni mkubwa ukiwemo wa kuunganisha ndege kwenda nchi nyingine.

Kagirwa alisema ATCL inaenda Lubumbashi mara tatu kwa wiki ikiwemo Jumanne, Alhamisi na Jumamosi na inaondoka saa tano asubuhi na kurudi saa kumi na moja jioni, lakini kuanzia Mei 4 mwaka huu, safari hizo zitaongezeka na itakuwa Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Jumamosi na pia wanajipanga kuanzisha safari za Kinshasa.

Hivi karibuni wakuu wa nchi EAC walikubali DRC iwe mwanachama wake. Kabla ya DRC, EAC ilikuwa na wanachama sita ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na Burundi.

Viongozi hao akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan walitoa uamuzi huo kupitia kura zilizopigwa wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao, ukiongozwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Mwenyekiti wa EAC, Rais Uhuru alitangaza uamuzi huo na akasema kukubalika kwa DRC kunaashiria tukio muhimu katika historia ya ushirikiano wa eneo hili la Afrika Mashariki.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaikaribisha kwa moyo mkunjufu DRC katika jumuiya. KAZI IENDELEE!,” alisema Rais Samia akiwa katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live