Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bandari DSM yaweka rekodi nyingine

5deebdf4135ab180697745a6c021091a.jpeg Bandari DSM yaweka rekodi nyingine

Fri, 10 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeingia katika historia nyingine baada ya kupokea meli ya Serene Theodore yenye shehena ya Sulphur tani 38,500.

Kiwango hicho cha kemikali hakijawahi kupokewa katika bandari hiyo kwa kipindi cha miaka 10.

Juni mwaka huu, meli ya TRANQUAIL ACE (IMO: 9561253) inayomilikiwa na Kampuni ya Mitsui ikitoka nchini Japan ilitia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa na magari 3,743 ambayo ni mengi zaidi kuwahi kusafirishwa kuja nchini kwa mara moja.

Mkurugenzi wa kampuni ya mizigo ya Epic Cargo iliyoratibu ujio wa mzigo huo wa Sulphur nchini, Anthony Swai alisema meli hiyo iliyotoka Doha, Qatar ilitia nanga juzi Septemba 8, saa mbili usiku.

Swai alisema malori zaidi ya 1,664 yatatumika kusafirisha mzigo huo kuupeleka Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na kwamba utatumika kwa kuchenjua madini.

“Hii ni rekodi kubwa kuwahi kufikiwa katika historia ya bandari zote za Tanzania. Mzigo mkubwa kama huu uliwahi kupokelewa miaka 10 iliyopita katika bandari ya Dar es Salaam, ukiwa na tani 30,000,” alisema.

Swai alisema mzigo huo umeiwezesha serikali kuingiza dola za Marekani milioni 2.2, sawa na Sh bilioni 5.101, na TPA katika tozo ya kuhifadhi mzigo iliingiza Sh milioni 260.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Erick Hamis alisema Juni mwaka huu meli iliyobeba Sulphur ani 15,000 ilitia nanga na kushusha mzigo huo lakini sasa imekuja meli iliyobeba mzigo wenye uzito mara mbili zaidi.

“Tunafanya kazi kwa umoja na viwango vya juu. Bandari zetu zinafanya kazi saa 24 huwezi kutofautisha usiku na mchana,” alisema.

Mkuu wa Usalama wa Bandari wa TPA, Mussa Biboze, alisema taratibu zote za kiusalama bandarini hapo zimefuatwa ikiwemo katika kushusha na kupakia Salfa hiyo na kusimamiwa na NEMC pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz