Balozi wa VietNam nchini Tanzania Nguyen Nam Tien aliyefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Mafia ameeleza kuvutiwa kwake na vivutio vilivyopo nchini ikiwemo Samaki aina ya Papa Potwe (whale shark).
Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhandisi Martine Ntemo ameelezea kuwa ziara hiyo imefanyika mwishoni mwa mwezi Septemba na imekuwa ya ufanisi kwani nchi ya Viet Nam ni moja kati ya mataifa ambayo yameweza kuboresha uchumi wake kwa kipindi kifupi kutoka kuwa nchi masikini hadi taifa lenye viwanda vingi.
Ntemo amesema Mafia ni kisiwa tajiri kwa mambo mengi ikiwemo kilimo cha nazi, uvuvi lakini chenye umaarufu mkubwa duniani na utajiri wa viumbe hai vinavyopatikana baharini kuzunguka kisiwa hicho.
Amesema vipo vivutio vingine ambavyo vimemshawishi balozi huyo kutembelea kisiwa cha Mafia ambavyo ni pamoja na samaki mkubwa mwenye urefu wa mita 18 na uzito wa tani 12 aitwaye Papa Potwe( whale shark), samaki huyu anapatikana sehemu chache duniani
“Hivyo vivutio ni kati ya vichache vilivyomvutia balozi wa Vietnam lakini pia Kisiwa hiki kina historia iliyosheheni mabaki ya ustaarabu wa kale hasa baada ya kubainika kuwa ndicho kilikuwa moja ya vituo muhimu vya wasafiri wa baharini tangu karne ya nane” ameelezai.
Amesema katika ziara hiyo Tien amepata fursa ya kujionea shughuli mbali mbali za kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo kilimo cha minazi na uzalishaji wa mafuta ya nazi.
“Balozi amepata fursa pia ya kutembelea sekta ya Nishati ya umeme niliweza kufanya mazungumzo naye kuhusu maeneo mahsusi ya ushirikiano ambayo nchi ya Viet Nam inaweza kutoa mchango wake kukabiliana na vikwazo vilivyopo ikiwemo kuboresha usafiri wa kukiunganisha kisiwa na upande wa bara kupitia wilaya za Kibiti, Lindi na jiji la Dar es Salaam” ameeleza Ntemo..
Ntemo amesema kwamba Balozi huyo amechukua vikwazo alivyoviona ili kuwaunganisha wawekezaji na wafanya biashara nchini kwao waweze kushiriki katika utatuzi wa changamoto hizo zilizopo katika kisiwa cha Mafia.