Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bakhressa wanausubiri mwongozo wa TCRA kwa hamu

12266 BAKRESA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 16 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uongozi wa Kampuni ya Bakhressa (BFPL) umesema unasubiri kwa hamu mwongozo utakaotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)   kuhusu ving'amuzi vilivyoondoa chaneli za ndani baada ya kukiuka masharti ya leseni.

Agosti 13 mwaka huu, Waziri wa Habari, Sanaa,Michezo,Burudani na Wasanii,Dk Mwakyembe aliitaka TCRA kutoa mwongozo  utakaosadia kampuni za visimbuzi za Azam, Zuku na DSTV zitakavyoweza kurusha maudhui ya ndani.

Hivi karibuni kampuni hizo zililazimika kuacha kurusha chaneli za ndani baada ya kukiuka masharti ya leseni zao ambayo yanawataka kurusha maudhui hayo kwa kuyalipia.

Meneja Uhusiano wa Bakhressa, Hussein Sufian ameiambia Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, leo Alhamisi Agosti 16, 2018 kuwa wanausubiri mwongozo huo.

Kamati hiyo ya Bunge imeelezwa hayo wakati ilipotembelea kiwanda cha kusindika matunda na kutengeneza juisi kilichopo Mlandenge wilayani Mkuranga.

Sufian ameeleza hayo wakati akitoa changamoto zinazoikabili kampuni hiyo na kusema hatua ya Serikali ya kuzitaka Azam kuondoa maudhui ya chaneli za ndani ni kuwaumiza wananchi.

"Tunausubiri kwa hamu mwongozo huu ili wananchi wetu waondokane na hali ya kumiliki visimbuzi viwili jambo ambalo ni mzigo kwao.

“Tunaamini busara itatumika zaidi kurejesha huduma kwa Watanzania na muafaka utapatikana wa suala hili na tuna imani na Serikali," amesema Sufiani.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya amesema wizara hiyo imelisikia jambo hilo na wanalifuatilia kwa ukaribu kwa sababu linahusu biashara.

"Tutalifuatilia ili kujiridhisha na hatimaye tupate muafaka. Sasa hivi popote panapohusu biashara lazima tufuatilie na hili la visimbuzi ni biashara pia," amesema Manyanya.

Chanzo: mwananchi.co.tz