Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajeti yapanua fursa sekta ya kilimo

62658 Pic+kilimo

Fri, 14 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Serikali ya Tanzania imetangaza kuongeza fursa za uzalishaji wa ndani, kupunguza ushuru wa forodha katika baadhi ya mazao na misamaha ya Kodi ya Ongezeko la thamani huku ikitangaza ahadi tano katika uendeshaji wa sekta ya kilimo nchini.

Fursa hizo ni pamoja na kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja katika mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho yanayohusisha mazao ya soya, mawese, Alzeti ili kuchochea uzalishaji wa ndani.

Eneo lingine ni kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye ngano baada ya nchi wanachama kuwa chini ya mahitaji ya soko huku ikihamasisha wakulima nchini kuingia katika fursa hiyo.   

Matumaini hayo yametolewa jana Alhamisi Juni 13, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2019/2020, ikiweka wazi mipango na matarajio yake katika kuimarisha na kukuza sekta ya kilimo nchini.

“Kama wote tunavyofahamu, sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa uendelezaji wa viwanda Tanzania kwa kuwa sehemu kubwa ya malighafi za viwanda zinatokana na kilimo. Katika kuimarisha sekta hii,” alisema Waziri Mpango.

“Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) hususan kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo, huduma za ugani, masoko, miundombinu wezeshi na tafiti, ikiwa ni pamoja na kupeleka fedha zaidi kwenye maeneo wezeshi kwa kilimo na kutoa nafuu za kikodi.”

Pia Soma

Waziri Mpango alisema Serikali itahamasisha tija na uzalishaji, kuendelea na utafutaji wa masoko, kupunguza kero kwa wakulima, kuimarisha bodi za mazao ya kilimo, kutoa unafuu wa kikodi na kuvutia wawekezaji viwanda watakaotumia malighafi za ndani ikiwamo mazao ya kilimo.  

Alisema hatua hiyo inayoajiri wananchi wengi na hasa waishio vijijini, inatokana na unyeti wa sekta ya kilimo katika ufanikishaji wa  ndoto ya uchumi wa viwanda.

“Serikali itaendelea kuimarisha bodi za mazao, kuboresha na kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya mazao ili kuviwezesha kupata mikopo ya kuwekeza kwenye shughuli mbalimbali za kilimo na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya mazao,” alisema.

Alisema bajeti hiyo iliyopitishwa kwa idadi ya wabunge wengi, imepunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 100 hadi 35 kwa mwaka mmoja katika sukari ya matumizi ya kawaida inayoagizwa kutoka nje kwa kibali maalumu ili kuziba pengo lililopo

Chanzo: mwananchi.co.tz