Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajeti ya kilimo yapaa kwa zaidi ya asilimia 100

Bashe Kilimo Bajeti Bashe akiwasilisha bajei ya wizara hiyo jana

Wed, 18 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huenda sekta ya kilimo ikapata msukumo mpya baada ya Serikali kuongeza bajeti katika wizara hiyo huku fedha nyingi zikielekezwa katika umwagiliaji, utafiti na kukuza masoko ya mazao ya wakulima.

Waziri Kilimo, Hussein Bashe aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 jana Mei 17, 2022 Bungeni jijini Dodoma amesema wizara yake inapanga kutumia Sh751.12 bilioni mwaka ujao.

Kati ya fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya mwaka ujao unaoanza Julai 1, 2022, Sh631.5 bilioni zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 155.34 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2021/22 ambayo ilikuwa Sh294.16 bilioni.

Hadi kufikia Aprili mwaka huu, wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh272,93 bilioni sawa na asilimia 92.78 ya bajeti yote iliyoidhinishwa mwaka 2021/22. Waziri Bashe amesema sehemu kubwa ya bajeti ya mwaka ujao itaelekezwa katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, miundombinu ya uhifadhi wa mazao, kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao, kuimarisha utafiti wa kilimo, uzalishaji wa mbegu na utoaji wa ruzuku kwa wakulima.

“Vilevile, bajeti ya mwaka 2022/23 imejielekeza katika kutoa ruzuku ya mbolea kwa mazao yote, kuendeleza mashamba makubwa na kuongeza ushiriki wa vijana kwenye kilimo na kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kugharamia sekta ya kilimo,” amesema Bashe.

Pia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 18.6 hadi tani milioni 20 na uzalishaji wa mazao yenye mahitaji makubwa hususan mazao ya alizeti, ngano na chikichi.

Kilimo ni moja ya sekta muhimu zinazotegemewa na Watanzania wengi kujipatia kipato kwa ajili ya kutunza familia na kuboresha maisha.

Ongezeko la bajeti linatoa matumaini kwa wakulima kuboresha kilimo chao na kukifanya cha kisasa kitakachowawezesha kuongeza uzalishaji na kutanua wigo wa masoko wa mazao yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live