Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajeti ya 2019/20 kuongezeka Sh600 bil

46437 Pic+bajeti Bajeti ya 2019/20 kuongezeka Sh600 bil

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali imepanga kuongeza bajeti yake kwa Sh600 bilioni tu kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Bajeti ya mwaka unaoishia Juni 30 ilikuwa Sh32.5 trilioni, lakini ya mwaka ujao imepanga kufikia Sh33.1 trilioni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa takwimu hizo wakati akiwasilisha kwa wabunge Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2019/2020.

Lakini kati ya fedha hizo, Serikali inatarajia kukusanya Sh23 trilionikutoka katika mapato ya ndani yakijumuisha halmashauri, wakati nakisi itajazwa na fedha nyingine zitakazotokana na wafadhili, mikopo nafuu na ya masharti.

Hii ni mara ya nne kwa Serikali ya Awamu ya Tano kusoma ukomo wa bajeti yake. Katika makadirio yake ya mwaka 2016/17 ilipanga bajeti ya Sh29.5 trilioni, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh7 trilioni ya bajeti iliyoachwa na Serikali ya Awamu ya Nne.

Kwa mikakati ya 2019/20, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuwa Sh22.2 trilioni na kati ya hizo zinazotokana na kodi ni Sh19.1 trilioni na mapato yasiyo ya kodi ni Sh3.1 trilioni, wakati mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh765.4 bilioni.

Mikopo ya ndani inakadiriwa kuwa Sh4.9 trilioni na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara inakadiriwa kuwa Sh2.3 trilioni na misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ni Sh2.7trilioni.

Dk Mpango alisema kati ya fedha hizo Sh20.8 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambayo yatajumuisha gharama za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwishoni mwa mwaka na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida, mishahara itakuwa Sh7.5 trilioni huku matumizi mengineyo ya uendeshaji yakipangiwa Sh3.57 trilioni.

Alisema matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh12.24 trilioni na kati ya hizo Sh9.73 trilioni ni fedha za ndani na Sh2.51 trilioni ni fedha za nje.

Dk Mpango alisema hadi kufikia Januari, washirika wa maendeleo walikuwa wametoa Sh144 bilioni kati ya Sh2.13 trilioni zilizoahidiwa katika bajeti ya mwaka 2018/19.

Dk Mpango alisema fedha hizo ni kati ya Sh12 trilioni ambazo zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh9.87 trilioni zikiwa ni fedha za ndani na Sh2.13 trilioni ni fedha za nje.

“Sh144 bilioni zilipokelewa kutoka kwa washirika wa maendeleo na kupelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara, taasisi na wakala wa serikali, sektarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa,” alisema Dk Mpango.

Alisema Sh3.8 trilioni zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Fedha za miradi ya maendeleo

Dk Mpango alisema wanatarajia kutoa Sh1.43 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, kama wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji katika Mto Rufiji (MW2,115), maarufu kwa jina la Stigler’s Gorge.

Dk Mpango alisema katika kipindi cha kati ya Julai 2018 na Januari, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya Sh13.7 trilioni na kati hizo, Sh10.96 trilioni zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 2.78 trilioni kwa ajili ya maendeleo.

“Mahitaji yaliyopewa kipaumbe katika utoaji wa fedha ni pamoja na ulipaji wa deni la Serikali, ikijumuisha Sh5.46 trilioni za michango ya mwajiri katika mifuko ya hifadhi ya jamii, huku Sh3.8 trilioni zikitumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema Mpango.

Alisema Sh3.8 trilioni zilitumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma.

Utekelezaji wa miradi

Akizungumzia utekelezaji wa miradi, Dk Mpango alisema kukosekana kwa umeme wa uhakika katika baadhi ya viwanda kumesababisha hasara na kushindwa kupanua uwekezaji.

Alisema changamoto nyingine ni baadhi ya makandarasi kuwa na uwezo mdogo wa kukamilisha kazi ipasavyo, mawasiliano hafifu baina ya wadau wa miradi hususani watekelezaji, waratibu na wasimamizi.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kutopatikana kwa fedha kwa wakati, hali ambayo imeathiri utekelezaji wa miradi kulingana na ratiba na kuongeza gharama. Alisema uchakavu wa miundombinu na mitambo katika miradi kulisababisha uzalishaji kuwa chini ya kiwango kinachotakiwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz